• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 4:31 PM
‘Serikali itawalipa wanamichezo kwa miezi miwili na wa tatu yatarajia mashirika na kampuni zitawafaa’

‘Serikali itawalipa wanamichezo kwa miezi miwili na wa tatu yatarajia mashirika na kampuni zitawafaa’

Na ABDULRAHMAN SHERIFF

JANGA la corona limesababisha timu kadhaa za taifa za michezo na wanamichezo kushindwa kwenda ng’ambo kushiriki kwenye mashindano ya kimataifa.

Waziri wa Michezo Balozi Amina Mohamed amesema janga la corona lilisababisha kuahirishwa hadi mwakani kwa michezo mikubwa na maarufu zaidi ni ile ya Olimpiki ambayo wanamichezo wa Kenya walikuwa wanaendelea na kujiandaa nayo.

Michezo hiyo ilikuwa ifanyike huko Tokyo nchini Japan. Michezo hii ya Olimpiki ni mikubwa, muhimu na maarufu ambayo kila nchi ilikuwa imeanza kujitayarisha kushiriki.

“Sisi Wakenya tulikuwa tumeingiza michezo mbalimbali kupigania medali pamoja na kudhihirisha kuwa tuna wanamichezo wenye kuipatia sifa na fahari nchi yao,” akasema Balozi Amina.

Michezo mingine ambayo Kenya ilikuwa ishiriki ni pamoja na yale ya vijana chini ya umri wa miaka 20 na yale ya riadha ambayo yalipangwa kufanyika mwezi wa Julai, Safari Rally ambayo nayo yameahirishwa mpaka mwakani.

Waziri Amina pia amesema serikali ilifikiria kuwasaidia wanamichezo ambao wameathirika kutokana na janga la corona na hivyo, imewapatia kila mmoja wakiwemo wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL) na Ligi Kuu ya Wanawake (KWPL) Sh10,000 kwa kipindi cha miezi miwili.

Alieleza matumaini yake kuwa kampuni za wamiliki binafsi na mashirika yatawasaidia kuwalipa wanaspoti hao kwa mwezi wa tatu ili wale walioathirika wapate kujisaidia wao pamoja na familia zao.

“Tunafahamu kuwa wanaspoti wanaume na wanawake wameathirika pakubwa kwa janga hili na hivyo, tukiwa aserikali tumeonelea tuwasaidie,” akasema Waziri Amina huku akiwataka wanamichezo kufanya mazoezi ya binafsi kujitayarisha kushiriki michezoni janga likiisha.

Balozi Amina amesema kwamba serikali inazingatia umuhimu wa michezo yote na wala si michezo fulani pekee bora uongozi wa mashirikisho ama vyama vya michezo iwe yenye kupeleka mambo yao kulingana katiba zao na kufuata mwongozo wa spoti.

“Tunashirikiana vizuri sana na vyama na mashiriksho ya michezo kote nchini. Ni juu ya maafisa wa michezo hiyo wafanye kila liwezekanalo kutimiza malengo yao na sisi upande wetu tutakuwa wenye kusaidia kwenye mambo yatakayohakikisha michezo inaendeshwa vizuri,” akasema waziri huyo.

Baadhi ya maafisa wa michezo wamempongeza Amina kwa jinsi anavyochukulia michezo kuwa ya umuhimu na anavyosaidia kuhakikisha timu zinazokwenda ng’ambo, zinasaidika na hazipati taabu zikiwa huko.

Rais wa Shirikisho la Tong-IL Moo-Do la Kenya, Clarence Mwakio alisema kuwa Waziri Amina amechukulia umuhimu wa wizara hiyo ya michezo na akaeleza imani yake kuwa Kenya itawika kwenye mashindano na michezo itakayofanyika baada ya janga la corona.

Rais wa Shirikisho la Tong-IL Moo-Do nchini Kenya, Clarence Mwakio. Picha/ Abdulrahman Sheriff

“Amina ametusaidia kwa mambo mengi wakati tuliposhiriki mashindano ya dunia huko mjini Chungju nchini Korea Kusini mwaka uliopita na pia wakati wa mashindano ya Mombasa Open yaliyofanyika mjini Mombasa mwishoni mwa mwaka jana,” akasema Mwakio.

Mwakio alieleza imani yake kuwa watafanya vizuri kwenye mashindano ya dunia ya mwaka huu ikiwa itafanyika baada ya corona kuangamizwa.

“Tuna imani kubwa serikali kupitia kwa Waziri Amina itatusaidia kwa safari yetu ya Thailand ikiwa mashindano yatafanyika,” akasema.

Mchezaji wa timu ya taifa ya mchezo huo wa Tong-IL Moo-Do, Lorna Abiero anasema yeye na wenzake wanafanya mazoezi kwa ajili ya kujiandaa kwa mashindano yanayotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu 2020.

“Tuna hamu ya kushiriki tena mashindano ya dunia ili tuweze kushinda medali nyingi zaidi za dhahabu, fedha na shaba. Tuna nia kubwa ya kubeba taji la mashindano hayo baada ya kumaliza nafasi ya pili mwaka 2019,” akasema Lorna.

You can share this post!

Wizara yafuatilia shughuli za ujenzi wa uwanja wa kisasa...

Arsenal yawafuta kazi maskauti waliochangia kusajiliwa kwa...

adminleo