Majonzi mtoto kuliwa na mamba
Na Alex Njeru
FAMILIA moja katika kijiji cha Majara, kaunti ndogo ya Tharaka Kusini inaomboleza kifo cha mtoto wao wa shule ya msingi aliyeliwa na mamba katika Mto Tana.
Babake mtoto huyo, Bw George Mutaba, alisema mwanawe alikuwa akinywa maji mtoni aliposhambuliwa na mamba aliyemvuta ndani ya maji.
Mvulana ambaye alikuwa na marehemu wakati wa tukio, alieleza kuwa alijaribu kumuokoa mwenzake kwa kumfuata mamba ndani ya maji lakini aliendelea kumvuta kwa sehemu ya maji mengi mtoni.
Chifu wa lokesheni ya Maragwa, Bw William Kwenda alisema wakazi walijaribu kusaka mabaki ya mtoto huyo bila mafaniklio.
Alisema maafisa wa Shirika la Wanyama Pori waliopo kwa Mbuga ya Kitaifa ya Meru walizuru mahali hapo na kuonya wakazi dhidi ya kuwaruhusu watoto wao kwenda mtoni ambapo mamba wamejaa.
Mkazi wa eneo hilo, Bw Njagi Mono alisema watoto watano pamoja na mamia ya mifugo wameliwa na mamba kijijini humo katika muda wa miaka michache.
Aliomba serikali iwawekee mifereji ili waweze kupata maji pamoja na kuwajengea sehemu ambapo mifugo itapata maji bila kulazimika kufika mtoni.