• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:33 AM
Kushuka kwa bei ya mafuta hakujapunguza gharama ya maisha

Kushuka kwa bei ya mafuta hakujapunguza gharama ya maisha

Na LEONARD ONYANGO

KWA kipindi cha miezi miwili sasa, Wakenya wamekuwa wakinunua mafuta kwa bei ya chini kuliko ilivyo kawaida.

Kwa mfano, mwezi uliopita, Mamlaka ya Kawi na Mafuta (EPRA) ilitangaza punguzo la karibu Sh10 na Sh20 kwa kila lita ya mafuta ya petroli na dizeli mtawalia.

Ongezeko la bei ya mafuta limekuwa likitumiwa kama kigezo cha kuongeza bei ya bidhaa muhimu kama vile vyakula, maji na umeme.

Mathalani, kampuni ya kusambaza kawi ya Kenya Power, imekuwa ikipandisha bei ya umeme kutokana na kisingizio cha kupanda kwa bei ya mafuta ya petroli na dizeli ambayo hutumika kuendesha jenereta zake zilizoko kwenye mabwawa mbalimbali nchini.

Kampuni za kusambaza maji pia zimekuwa zikitumia kigezo cha bei ya juu ya mafuta na ukame kuongeza gharama ya maji. Lakini sasa bei ya mafuta imeteremka na mvua inanyesha lakini bei ya maji inaendelea kuongezeka.

Ripoti kuhusu bei ya bidhaa iliyotolewa wiki iliyopita na Shirika la Takwimu (KNBS), inaonyesha kuwa bei ya bidhaa muhimu iliongezeka kwa kiasi kikubwa kati ya Aprili na Mei mwaka huu.

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa bei ya umeme, maji, gesi ya kupikia iliongezeka katika kipindi hicho. Kwa mujibu wa ripoti, ongezeko hilo linatokana na kuongezeka kwa bei ya mafuta ya taa. EPRA iliongeza bei ya mafuta ya taa kwa Sh2.49 mwezi uliopita.

Bei ya vyakula kama vile sukumawiki, maharagwe, spinachi, machungwa, karoti, vitunguu na vinywaji visivyokuwa na vileo nayo imekuwa ikiongezeka kwa kasi tangu Aprili, kwa mujibu wa ripoti ya KNBS.

Wataalamu wa masuala ya uchumi walikuwa wametabiri kuwa kupungua kwa bei ya mafuta kungepunguza gharama ya uzalishaji na usafirishaji wa bidhaa, hivyo kuwapa Wakenya afueni.

Jambo la kushangaza ni kwamba Wakenya wanaendelea kuumia kutokana na bei ya juu ya bidhaa badala ya kupata afueni iliyotarajiwa.

Ni kweli kwamba janga la virusi vya corona limetatiza uzalishaji. Lakini janga hilo halifai kulaumiwa kwa kuongezeka kwa bei ya bidhaa muhimu kama vile maji na umeme.

Serikali imekuwa ikilaumu wamiliki wa magari ya umma kwa kuendelea kuwatoza abiria nauli ya juu licha ya bei ya mafuta kupungua. Lakini kwa upande wake, serikali pia imeshindwa kuwapunguzia mzigo mzito Wakenya wa gharama ya juu ya umeme, maji na vyakula.

You can share this post!

Majonzi mtoto kuliwa na mamba

Hujuma polisi kuacha jeneza barabarani

adminleo