Mashakani kwa kujifanya waajiri hospitalini
TITUS OMINDE
Watu wawili washtakiwa kwa ulaghai baada ya kumhadaa mwanabiashra mmoja na kupata Sh200,000 kwa madai kwamba wangemsaidia mwanawe kupata kazi ya uuguzi katika Hospitali ya Mafunzo ya Moi.
Watuhumiwa hao wanasemekana kujifanya kuwa mkurungezi mtendaji wa hospitali hiyo, Dkt Wilson Arausa.
Zacharia Kiprotich Sang na Benard Cheruiyot Rotich walishtakiwa mbele ya hakimu mkuu wa korti ya Eldoret Christine Menya.
Mshukiwa mwingine aliachiliwa huru baada ya kukosekana kwa ushaidi wa kutosha.
Mashtaka ya kwanza ni kwamba wawili hao pamoja na wengine walipokea Sh109,000 mnamo Aprili 11, 2020 kwa njia ya udanganyifu kutoka kwa Bi Alice Njeri Khiu mji wa Nakuru kupitia mpesa.
Mashtaka ya pili yalisema kwamba walichukua Sh108,500 kwa kujifanya wangemsaidia mwanawe Sarah Wanjiru kupata kazi ya uuguzi katika hospitali hiyo.
Upande wa mashtaka uliambia mahakama kwamba Machi 15, 2020 wawili hao walipata pesa kupitia njia zizizo halali kutoka kwa mtu mwingine – Vivian Chepchirchir Sh12,000 kwa kujifanya kuwa wangempa kazi katika hospitali hiyo.
Walishtakiwa kwa kujifanya mkurungezi mtendaji wa hospitali hiyo kwa kutumia akaunti ya mitandao yenye jina Dkt Aruasa Wilson mwezi wa Februari 14,2020 mji wa Eldoret.
Washukiwa hao walikamatwa Mei 21, 2020 na kuwekwa kizuizini katika kituo cha polisi cha kaunti ndogo ya Turbo. Walikuwa wamewakilishwa na mwanasheria Elijah Ayieko. Walikanusha mashtaka hayo na kuachiliwa kwa dhamana ya Sh200,000.