Wachezaji wa Gor hawajalipa kodi kwa miezi 5 – Rachier
CHRIS ADUNGO
WAKILI Ambrose Rachier ambaye ni mwenyekiti wa Gor Mahia, amesema miamba hao wa soka ya humu nchini wanapitia hali ngumu zaidi ya kifedha na wameshindwa kulipa mishahara ya wachezaji wao kwa muda wa miezi mitano iliyopita.
Kwa mujibu wa Rachier, hali mbaya ya kifedha ya Gor Mahia imemweka katika ulazima wa kuandikia barua ‘malandlodi’ wa baadhi ya wanasoka wa K’Ogalo ili wasiwafurushe kwa sababu ya kukosa kulipa kodi za nyumba mwishoni mwa kila mwezi.
“Nimekuwa nikiwaandikia wamiliki wa nyumba ambazo wachezaji wetu wanaishi ili wasiwahangaishe wanaposhindwa kulipa kodi. Nashukuru kundi la malondlodi ambao wameelewa hali yetu na kusamehe kodi za baadhi ya wanasoka hao au kurefusha kipindi cha malipo husika,” akasema Rachier kwa kukiri kwamba hawajalipa pia wachezaji wao mshahara wa Mei 2020.
Licha ya panda-shuka hizo za Gor Mahia, Rachier na wachezaji watatu wa mabingwa hao mara 19 wa taji la KPL walijumuika na kundi la mashabiki wao liitwalo Kulundeng ili kuwasaidia watu wasiojiweza katika eneo la Kawangware, Nairobi.
Zaidi ya familia 50 zilinufaika kwa misaada ya chukala kutoka kwa wahisani walioshirikiana na Gor Mahia.
Wito wa Rachier unatolewa siku chache baada ya serikali kutoa Sh10,000 kwa kila mmojawapo wa wachezaji wa klabu 12 za KPL kwa kipindi cha miezi mitatu ijayo.
Fedha hizo zinazonuia kuwapiga jeki wakati huu wa janga la corona ni sehemu ya mgao wa Sh20 milioni kutoka kwa Hazina ya Kitaifa ya Michezo.
Maagano ya kutolewa kwa fedha hizo yaliafikiwa wiki chache zilizopita kwa azma ya kuwasaidia wachezaji ambao wamekuwa wakikabiliana na hali ngumu ya kimaisha baada ya michezo iliyokuwa kitega-uchumi kwao kuahirishwa kwa sababu ya corona.
Vikosi vya pekee vya KPL ambavyo vilikosa mgao huo ni Bandari, Posta Rangers, Tusker, Ulinzi Stars na wanabenki wa KCB.