Makala

SIHA NA LISHE: Umuhimu wa kula saladi

June 2nd, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na MARGARET MAINA

[email protected]

SALADI ni mchanganyiko wa matunda na mboga mbichi.

Ulaji wa mbogamboga zikiwa katika hali ya ubichi au zikiwa hazijapikwa una faida kubwa kiafya.

Hata hivyo, ulaji huo bila ya kuchukua tahadhari unaweza kusababisha magonjwa yanayoenea kutokana na kula vyakula vichafu visivyosafishwa vema.

Mboga za majani ambazo hazijakomaa na mbichi ni chanzo kikubwa cha vitamini na madini ya aina mbalimbali.

Mboga hizo endapo zitakamuliwa na kutumiwa kama juisi, faida kiafya zitakuwa chungu nzima hasa kwa wagonjwa.

Mboga za majani za kijani ni chanzo kikubwa cha carotene ambayo inabadilishwa mwilini na kuwa vitamini A. Pia, ni chanzo kizuri cha vitamini C.

Vitamini A ina kazi kubwa ya kuimarisha macho ili yaone vizuri hasa wakati wa giza. Mbogamboga pia, husaidia kuimarisha kinga ya mwili.

Vitamini C ina kazi nyingi ikiwemo kuimarisha kinga, kuponya mafua na vidonda.

Baadhi ya mbogamboga zina protini na wanga. Kwa mfano, maharagwe na kunde ni chanzo kikubwa cha madini ya chuma na protini.

Viazi mviringo na viazi vitamu ni chanzo kikubwa cha wanga mwilini. Watu wanashauriwa watumie mboga mbichi kama vile saladi na kachumbari wakati maankuli.

Wanaweza kuzitumia zikiwa zimekatwakatwa au kusagwa ili kupata juisi, lakini ni lazima kuzingatia usafi wakati wa kuandaa mboga hizo.

Ulaji wa vyakula vibichi ambavyo havikuoshwa vizuri ni chanzo kikubwa cha magonjwa ya kuambukiza kama vile homa ya matumbo, kipindupindu, kuharisha, kupata minyoo na amiba.

Kwa sababu hiyo, watu wanashauriwa kuosha vizuri mbogamboga kwa kutumia maji safi. Pia, watu wale saladi na wanywe juisi ya mboga mbichi ili kupata virutubisho vingi zaidi.

Mbogamboga kama matango, nyanya na karoti, zitumike kutengeneza juisi bila ya kuondoa maganda yake kwa sababu yana madini na protini kwa wingi.