• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 5:55 AM
Afueni kwa wafanyabiashara wa Mombasa

Afueni kwa wafanyabiashara wa Mombasa

Na WINNIE ATIENO

WAFANYABIASHARA wadogo wapatao 1,000 Mombasa wamepata afueni baada ya serikali hiyo ya kaunti kuahidi kupunguza kodi kwa asilimia 50 ili wamudu sekta hiyo.

Aidha kupunguzwa kwa ada kutawasaidia kupambana na hali ngumu ya maisha iliyosababishwa na janga la corona.

Biashara kadhaa zimeathirika kutokanna na janga hilo hususan sekta ya utalii ambayo ndiyo kitovu cha uchumi wa Mombasa.

“Tunataka kuwasaidia wafanyabiashara ambao wanapitia hali ngumu kimaisha na ndiyo maana tumeamua kuwapunguzia ada kwa asilimia 50. Kama serikali ya kaunti tutasimama na wafanyabiashara hadi pale tutakapokabiliana na janga hili,” alisema Spika wa Bunge la Mombasa Bw Aharub Khatri.

Akiongea na Taifa Leo, Bw Khatri alisema bunge la kaunti pia linajadili namna ya kuokoa sekta ya uchukuzi ambayo pia inaendelea kukadiria hasara baada ya magari mengi kuegeshwa.

“Idara ya fedha inapania kuwapunguzia au kuwaondolea ada za maegesho katika sehemu za umma hususan matatu na tuktuk kwa miezi mitatu ambayo tumekuwa tukikabiliana na janga la corona; Machi, Aprili na Mei,” alisema.

Muungano wa wamiliki wa matatu umepongeza serikali ya kaunti kwa hatua hiyo ukisema wamiliki wamekuwa wakijaribu kuwasiliana nao ili wawasaidie.

Mshirikishi wa wamiliki wa wenye matatu tawi la Pwani Bw Salim Mbarak alisema asilimia 50 ya magari ya uchukuzi wa umma yameegeshwa kutokana na janga la corona.

Alisema wafanyabiashara hao wanaendelea kukadiria hasara huku wamiliki wengi wa matatu wakiamua kusitisha biashara hiyo kwa muda hadi pale mambo yatarejea kawaida.

Kuna zaidi ya matatu 6,000 eneo la Pwani.

Kila mwezi wamiliki hao hulipa Sh2,000 Kaunti ya Mombasa kama ada ya kuegesha magari yanapohudumu barabarani.

“Tunaunga mkono serikali katika jitihada ya kukabiliana na corona. Tutaendelea kuhimiza abiria wetu wasikusanyike kwa matatu,” alisema Bw Mbarak.

Matatu ya kubeba abiria 14 kwa sasa inabeba wanane ili kuzuia maambukizi ya virusi hivyo.

Alisema awali walikuwa wanapata faida ya Sh3500 au Sh5000 kwa siku lakini kwa sasa hali imekuwa ngumu.

You can share this post!

Serikali ya kaunti ya Kwale yaweka mikakati kufungua...

Uhuru amtembeza Raila jijini usiku

adminleo