Wanafunzi 2600 wakataa digrii, wajiunga na taasisi za kiufundi
Na WANDERI KAMAU
WANAFUNZI 2,632 ambao walihitimu kujiunga na vyuo vikuu kwenye Mtihani wa Kidato cha Nne (KCSE) mwaka uliopita, wameamua kujiunga na Taasisi za Kiufundi (TVETs), amesema Waziri wa Elimu Prof George Magoha.
Idadi hiyo ni ongezeko la wanafunzi 1, 363 ikilinganishwa na 2018, ambapo wanafunzi 1,269 waliamua kujiunga na taasisi hizo, licha ya kufikisha alama ya C+ inayohitajika kwa wao kujiunga na vyuo vikuu.
Akitoa ripoti kuhusu idadi ya wanafunzi watakaojiunga na vyuo vikuu na vyuo anuwai mwaka huu jana, Prof Magoha alisema kuwa mkondo huo unadhihirisha kuongezeka kwa umaarufu wa taaluma za kiufundi miongoni mwa wanafunzi.
“Kadri siku zinavyoenda, kozi za kiufundi zinazofunzwa katika vyuo anuwai zinazidi kukumbatiwa na wanafunzi. Hii ni baada ya kubaini kuwa, si lazima wawe na shahada kutoka vyuo vikuu ili kufanikiwa maishani,” akasema.
Kulingana na ripoti hiyo, jumla ya wanafunzi 122, 831 walipata nafasi za kujiunga na vyuo vikuu vya umma, huku 88,724 wakipata nafasi za kujiunga na vyuo anuwai.
Idadi hii ni kati ya nafasi 145, 129 zilizotangazwa na vyuo vikuu huku vya anuwai vikitangaza nafasi 276, 163.
Vyuo anuwai
Kulingana na Wizara ya Elimu, kati ya wanafunzi 88,724 watakaojiunga na vyuo anuwai, 53, 726 watafanya kozi za kiwango cha diploma, 29,112 viwango vya shahada huku 5,886 wakifanya kozi za kiufundi katika kiwango cha vyeti maalum.
Jumla ya wanafunzi 687,007 walifanya mtihani wa KCSE mwaka uliopita, ambapo 125,463 walihitimu kujiinga na vyuo vikuu.
Kulingana na serikali, vyuo anuwai viko wazi kuwapokea wanafunzi waliofanya mtihani wao wa KCSE mwaka uliopita na hata miaka ya nyuma hadi 1994.
Waziri alisema kuwa wanatarajia idadi hiyo kuongezeka zaidi baada ya kupokea idadi ya wanafunzi waliojiunga na taasisi hizo moja kwa moja.
“Kando na hayo, Idara ya Kuwaweka Wanafunzi katika Vyuo Vikuu na Vyuo Anuwai (KUCCPS) huwa inawatuma wanafunzi katika vyuo hivyo katika nyakati mbalimbali za mwaka,” akasema.
Ili kufahamu kozi ambazo watasomea kwenye vyuo vikuu, wanafunzi wameshauriwa kuangalia katika tovuti ya KUCCPS kwa kutumia namba zao za usajili wa mitihani.
Na kati ya vyuo vikuu vyote 68 nchini, Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia (JKUAT) katika eneo la Juja kilipokea wanafunzi 6,006 hiyo ikiwa idadi kubwa zaidi.
Vyuo vingine vilivyochukua idadi kubwa ya wanafunzi ni Chuo Kikuu cha Kenyatta, Nairobi na Moi (Eldoret).
Licha ya idadi hiyo, baadhi ya kozi katika vyuo hivyo hazikupata mwanafunzi hata mmoja, hali iliyomlazimu waziri kuviamuru kutathmini upya ufaafu na ushindani wa kozi husika.