Makala

WASONGA: Mabadiliko ya katiba hayatamaliza ghasia

June 3rd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

MAUDHUI kuu katika hotuba ya Rais Uhuru Kenyatta wakati wa maadhimisho ya Sikuu Kuu ya Madaraka mnamo Jumanne wiki hii ilikuwa ni mabadiliko ya Katiba.

Rais alielezea matumaini kuwa mageuzi ya katiba yatasaidia kukomesha msururu wa ghasia ambazo hushuhudiwa nchini kila baada ya chaguzi mkuu tangu mwaka wa 1992.

Aidha, alisema mageuzi hayo yatatusaidia kuimairisha misingi ya demokrasia yetu ili kuhakikisha tumejenga nchi ambayo jamii zote zinahisi kushirikishwa katika asasi za uongozi.

Lakini sikubaliani na Rais Kenyatta kwamba suluhu kwa fujo za kila baada ya miaka mitano au baadhi ya jamii za nchi hii kuhisi kutengwa uongozini ni mabadiliko ya katiba hii.

Sikushawishika na kauli yake kwamba tunapaswa kurekebisha sehemu zenye kasoro katika Katiba hii ambayo ilizinduliwa mnamo mwaka 2010.

Sababu ni kwamba kote duniani hamna Katiba ambayo inaweza kutajwa kama bora zaidi na isiyo na dosari zozote.

Kile ambacho hupelekea Katiba fulani kuonekana mbaya ni pale inapotumiwa vibaya na viongozi waliopotoka kimaadili.

Viongozi wasiojali maslahi ya raia wa kawaida, bali yale ya wandani wao wachache na watu kutoka makabila yao.

Ama kwa hakika, hii ndiyo maana japo Kenya na mataifa kama vile Malaysia na Singapore yalikuwa katika kiwango kimoja kimaendeleo mnamo 1963, nchi hii imesalia nyuma ikilinganishwa na mataifa hayo ya bara Asia.

Licha ya kuwa na umri mkubwa, Waziri Mkuu wa sasa wa Malaysia, Bw Mahathir bin Mohammed alichaguliwa tena mnamo 2018 kwa sababu chini ya uongozi wake, kati ya 1981 hadi 2003, uchumi wa taifa hilo ulinawiri zaidi.

Ni vigumu zaidi kwa hali kama hii kushuhudiwa nchini Kenya kwa sababu viongozi wetu wa hapo nyuma walitumia katiba kujifaidi wao wenyewe, wandani wao na watu wachache kutoka makabila yao.

Kwa mfano, ukweli ni kwamba mbegu za ukabila na ufisadi zilipandwa nchini chini ya uongozi wa Hayati Mzee Jomo Kenyatta.

Baadaye ziliota na kinyunyiziwa maji chini ya utawala wa Hayati Mzee Daniel Moi kupitia kwa falsafa yake ya “kufuata nyayo”.

Na licha ya kwamba marehemu Tom Mboya alikuwa kiongozi shupavu, yeye ndiye aliyeandaa sera ya maendeleo maarufu kama “Sessional Paper No 10” ya 1965.

Ni chini ya sera hiyo ambapo baadhi ya maeneo nchini, kama vile, Kaskazini na Kaskazini Mashariki yalitengwa kimaendeleo eti kwa sababu ni kame.

Isitoshe, maeneo walikotoka viongozi wa kisiasa ambao walipinga utawala wa Kanu enzi hizo yalitengwa kimaendelea.

Wananchi wa kawaida walielekezwa kuamini kuwa maeneo ambako Rais alitoka au ambako viongozi wake walisifu chama tawala ndiyo yaliyofaidika kwa miradi ya maendeleo kama vile ujenzi wa barabara nzuri na usambazaji wa stima.

Kinaya ni kwamba hata baada ya Katiba ya sasa iliyoanzisha utawala wa ugatuzi, bado kuna raia walioelekezwa kuamini kuwa “chimbuko” la maendeleo ni urais.

Kwa hivyo, mtazamo ni kwamba hisia kama hizi zinazoletwa na uongozi mbaya uliopotoka kimaadili, ndizo huchangia katika ghasia kutokea kila baada ya chaguzi kuu wala sio dosari katika katiba.

Katiba hii itaifaidi taifa hili pakubwa ikiwa viongozi watabadili mitazamo yao na kuelewa kuwa nyadhifa wanazoshikilia ni mali ya makabila yote 43 nchini wala sio makabila wanakotoka.

Mabadiliko ya Katiba yenye lengo la kubuni nafasi ziadi za uongozi kama inayoependekezwa kwenye ripoti ya BBI hayasaidia taifa hili