Mudavadi bado ndiye msemaji wetu – Atwoli
Na WANDERI KAMAU
KATIBU Mkuu wa Chama cha Kitaifa cha Wafanyakazi (COTU), Bw Francis Atwoli, amesema kuwa angali anamtambua kiongozi wa chama cha Amani National Congress (ANC), Bw Musalia Mudavadi, kama kiongozi rasmi wa kisiasa wa jamii ya Abaluhya.
Bw Atwoli pia amesema kuwa hana uhasama wowote na kiongozi huyo, baada ya hali ya kutoelewana kuonekana kuibuka kati ya viongozi hao wawili.
Kauli yake inajiri baada ya Bw Mudavadi na kiongozi wa Ford-Kenya, Bw Moses Wetang’ula, kukosa kuhudhuria mkutano wa karibu viongozi 40 kutoka eneo la Magharibi uliofanyika katika makazi ya Bw Atwoli, Kaunti ya Kajiado, Jumamosi iliyopita.
Lakini kwenye mahojiano jana, Bw Atwoli alisema kuwa Bw Mudavadi bado ndiye kiongozi wa kisiasa na msemaji rasmi wa jamii hiyo tangu kutawazwa rasmi mnamo 2017.
“Sina uhasama wowote na Bw Mudavadi. Ndiye amekuwa kiongozi wa kisiasa wa Abaluhya tangu 2017, alipotawazwa rasmi katika uwanja wa Bukhungu, Kakamega. Hilo halijabadilika,” akasema Bw Atwoli.
“Ikiwa mkutano huo ulikuwa wa Abaluhya, basi ungewashirikisha viongozi wa jamii hiyo pekee. Hata hivyo, ulikuwa wa viongozi wa eneo la Magharibi, ambalo linazishirikisha jamii nyingine kama Wateso,” akasema.
Alieleza kuwa ni sababu hiyo, ambapo kulikuwa na viongozi kama Gavana Sospeter OJaamong wa Busia, anayetoka katika jamii ya Teso.
Baadhi ya viongozi wengine waliohudhuria ni Waziri wa Ugatuzi Eugene Wamalwa, Gavana Wycliffe Oparanya (Kakamega), Seneta Cleophas Malala (Kakamega) kati ya wengine.
Tangu mkutano huo uandaliwe, Mabw Mudavadi na Wetang’ula wamemkosoa vikali Bw Atwoli, wakidai kuwa anatumia ushawishi wake kumpigia debe kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga, katika nia yake ya kuwania urais mnamo 2022.
Wawili hao pia wamemlaumu Odinga kwa kutumia ushawishi wake kuingilia uongozi wa Ford-Kenya, ambapo kundi moja lilidai kumwondoa Seneta Wetang’ula (Bungoma) kama kiongozi wake.
Lakini jana, Bw Atwoli alijitenga na madai hayo, akisema kuwa lengo lake kuu ni kushinikiza umoja miongoni mwa viongozi wa Magharibi, hasa mchakato wa Mpango wa Maridhiano (BBI) unapokaribia kurejelewa.
Alisema kuwa ataandaa mkutano wa pili katika uwanja uo huo, ili kutathmini uongozi wa jamii hiyo.
“Lengo langu kuu kwa sasa ni kuona kuwa eneo la Magharibi limeungana ili kutojipata nje ya serikali tena. Katika siku zijazo, nitaitisha mkutano mwingine katika uwanja uo huo ili kutathmini uongozi na mwelekeo wa kisiasa wa jamii ya Abaluhya,” akasema.
Kiongozi huyo vile vile alijitetea dhidi ya madai ya kuwatelekeza wafanyakazi na kujiingiza katika siasa, akisema kuwa masuala hayo mawili yana mwingiliano mkubwa.