• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:40 PM
Duale apuuza jaribio la kumng’oa afisini

Duale apuuza jaribio la kumng’oa afisini

Na CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Aden Duale amewapuuzilia mbali wabunge ambao wanadaiwa kukusanya sahihi za kumwondoa afisini.

Mnamo Jumatano Mbunge huyo wa Garissa Mjini aliwaambia wabunge hao wanaongozwa na Mbunge wa Kieni Kanini Kega kwamba waheshimu uamuzi wa Rais Uhuru Kenyatta kumduminisha katika wadhifa huo.

Bw Kega amedai kuwa kufikia Jumatano alikuwa amekusanya sahihi 117 akiongeza kuwa lengo lake ni kupata jumla ya sahihi 170.

Bw Duale alisazwa wakati ambapo shoka la Rais liliwaangukia jumla ya wabunge 16 wandani wa Naibu Rais William Ruto katika Bunge la Kitaifa wakati na baada ya mkutano wa kundi la wabunge wa Jubilee (PG) uliofanyika katika Ikulu ya Nairobi Jumanne.

“Ninafahamu kuwa Kega anakusanya sahihi kuniondoa afisini na hivyo kukiuka uamuzi wa Rais na Kiongozi wa chama,” Bw Duale akasema kwenye taarifa.

Alisema kuwa wabunge 212 ambao waliohudhuria mkutano huo waliinisha uamuzi wa kumdumisha katika wadhifa wa kiongozi wa wengi “na Kega na wenzake hawana mamlaka ya kubadili uamuzi huo.”

“Wale ambao wanakusanya sahihi wanafanya kazi bure kwa sababu sheria za bunge zimeelezea wazi taratibu za kuondolewa kwa Kiongozi wa Wengi,” Bw Duale akasema

Kulingana na sheria hizo sharti hoja hiyo iungwe wa chama chenye wabunge wengi katika mkutano wa kundi la wabunge, chini ya uongozi wa Kiongozi wa Chama.

Duale anashikilia kuwa utaratibu unahitaji kuwa uamuzi wa mkutano uwasilishwe na Kiranja wa Wengi kwa Spika.

“Hamna nafasi ya ukusanyaji wa sahihi. Ama kwa hakika mchakato huo ulikamilisha jana (Jumanne) katika mkutano ulioongozwa na Rais na ambao Kanini Kega pia alihudhuria,” Mbunge huyo wa Garissa Mjini akasema.

“Tumezoea sarakasi zake na vitisho na hatutashawishika. Mbona mbunge huyo ambaye anahudumu muhula wa pili na ambaye anafahamu utaratibu wa kuondolewa kwa Kiongozi wa Wengi anajifanya mjinga kwa kudai anakusanya sahihi?” akauliza.

Awali Mbunge wa Nyeri Mjini Ngunjiri Wambugu alisema: “Ikiwa Rais alitaka Duale aende, Duale angeenda. Rais aliamua kutomwondoa-kwa sababu ambazo yeye (Rais) anafahamu,”

“Ikiwa leo Rais ataamua kwamba Duale anapasa kuondolewa, hatadumu katika afisi hiyo kwa muda wa saa moja. Chama kitatekeleza hatua hiyo. Rais hahitaji sahihi zetu kabla ya kumwondoa Duale.”

Ni katika mkutano huo wa PG katika Ikulu ya Nairobi, uliohudhuriwa pia na Naibu Rais William Ruto ambapo uamuzi wa kuwaondoa Mbunge wa Mumias Mashariki Benjamin Washiali na Mbunge Maalum Cecily Mbarire walitemwa.

Washiali alipoteza kiti cha kiranja wa wengi uliomwendea Mbunge wa Navakholo Emmanuel Wangwe huku Bi Mbarire akivuliwa cheo cha naibu kiranja wa wengi uliomwendea Richar Maoke Maore (Mbunge wa Igembe Kaskazini).

You can share this post!

Mahangaiko mitaani watu wakikosa kodi

Serikali yawazia kufungua biashara Jumamosi

adminleo