• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Waandishi wa Afrika walaani mauaji ya George Floyd

Waandishi wa Afrika walaani mauaji ya George Floyd

Na HASSAN WEKESA

WAANDISHI zaidi ya 100 wa Afrika wasiojali mipaka ya kijiografia wameelezea kero yao kuhusu mauaji ya George Floyd yaliyotokea Mei 25 baada ya polisi mzungu kumbigija shingoni kwa goti mjini Minneapolis, Minnesota, Amerika.

Kwenye barua ya wazi wamelaani vitendo vya kikatili dhidi ya Waafrika-Waamerika.

“Tunayakumbuka kwa huzuni kubwa maneno aliyosema Malcom X mwaka 1964 alipokuwa Ghana, ‘Kwa milioni ishirini tulio na asili ya Afrika ambao tunaishi Amerika, kwetu sisi si ndoto ya ki-Amerika bali ni jinamizi.’ Kauli hii imebaki kuwa ni ukweli kwa Waafrika-Waamerika 37 milioni, mpaka katika mwaka huu wa 2020,” inasema sehemu ya barua hiyo ya wazi.

Barua hiyo ya wazi imepewa anwani ‘George Floyd: Waandishi wa Afrika wasiojali mipaka ya kijiografia Tuko Pamoja na Waafrika-Waamerika’.

Inataja wahanga wa mauaji ya kidhalimu kuwa ni George Floyd, Sandra Bland, Amadou Diallo, Matthew Ajibade, Eric Garner, John Crawford III, Michael Brown, Ezelll Ford, Dante Parker, na Michelle Casseaux, na wengine wengi ambao hawakutajwa, lakini “wanawakilisha watu wenye asili moja na sisi.”

Waliotia sahihi ni Abdilatif Abdalla, Mukoma wa Ngugi, Moses Kilolo, Yvonne Adhiambo Owuor, Troy Onyango, Precious Colette Kemigisha, Chris Abani, Noviolet Bulawayo, Leila Aboulela, na Angela Makholwa miongoni mwa wengine.

Waandishi hao wanaunga mkono maandamano ya kupinga ukandamizaji wa haki za binadamu ambayo yameingia wiki ya pili Amerika.

Haya yanajiri huku Derek Chauvin, 44, aliyembana Floyd kwa takriban dakika tisa na kusababisha kifo chake, akibadilishiwa mashtaka Jumatano kutoka kuua bila kukusudia hadi kitendo sawa na mauaji. Huenda akafungwa jela miaka 40.

Maafisa wengine watatu walioachishwa kazi pamoja na Chauvin nao wameshtakiwa kwa kusaidia kutekeleza mauaji. Upasuaji maiti umebainisha Floyd alifariki kwa kukosa hewa baada ya kukandamizwa shingoni kwa goti la afisa.

Floyd alikumbana na mauti yake mara alipoenda dukani kununua pakiti ya sigara na mhudumu akashuku kwamba alilipa akitumia pesa bandia kiasi cha dola 20 sawa na Sh2,000

Muuzaji huyo aliwaita maafisa wa polisi waliomkamata na kumtendea unyama huo.

Leo Alhamisi kunafanyika ibada ya heshima za mwendazake katika eneo la mkasa, huku mazishi yakitarajiwa Houston, Texas wiki ijayo.

Aliaga dunia kipindi kigumu akiwa hafanyi kazi ya ubaunsa aliyokuwa ameajiriwa kwa sababu ya changamoto zilizoletwa na janga la Covid-19.

You can share this post!

Waiguru akataa kuidhinisha fedha za ziada kwa bajeti ya...

‘Wakenya milioni moja wamepoteza kazi’

adminleo