Habari Mseto

'Wakenya milioni moja wamepoteza kazi'

June 4th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

NA PAUL WAFULA

WAKENYA wapatao milioni moja wamepoteza ajira au kuwekwa kwa likizo isiyo na malipo kutokana na makali ya ugonjwa wa Covid-19.

Mahojiano mengi pamoja na taarifa kuhusu wafanyakazi za kamupni nyingi nchini zinaashiria kuwa huenda wananchi zaidi ya milioni moja wamepoteza riziki, hasa wanaofanya kazi za sulubu wakihesabiwa.

Kwa mfano, mwanakandarasi anayejenga reli ya kisasa (SGR) aliwasimamisha kazi Wakenya 4,013 na Wachina 471 kutokana na hali mbaya ya kiuchumi.

Sekta zilizopata pigo zaidi ni utalii, uchukuzi, biashara ya maua, mawasiliano, viwanda, elimu, afya na hata kilimo.

Katika kampuni ya Kenya Airways, wimbi la kutimuliwa kazini linasheheni huku wafanyakazi 4,000 wakisubiri kampuni hiyo  inayorekodi hasara kila mwaka kupigwa jeki na serikali, na kuondolewa kwa marufuku ya huduma za ndege. Malipo ya wengi wa wafanyakazi yalipunguzwa kwa asilimia 75.

Hapo Machi, shirika la Bridge International liliwasimamisha kazi mamia ya walimu na kuwatuma kwa likizo ya lazima isiyo na malipo.

Hali ni sawa kwa shule 1932 za upili za kibinafsi na zingine 8,000 za kibinafsi za msingi ambazo zimechukua hatua hiyo.