Norfolk yabatilisha uamuzi wa kutimua wafanyakazi wote
Na SAMMY WAWERU
Kampuni ya Fairmont inayomiliki mikahawa kadhaa nchini imetangaza kubatilisha uamuzi iliyochukua kuwafuta wafanyakazi wake wote wa Mkahawa wa Norfolk, Nairobi.
Aidha, kampuni hiyo imesema imeafikia hatua ya kusimamisha kufuta wafanyakazi hao ili kushirikisha wadau husika wengine.
Mei 27, 2020, Fairmont ilitangaza kufunga Mkahawa wa Norfolk, Nairobi na kusimamisha kazi wahudumu wake.
Kwa mujibu wa notisi ya usimamizi wa kampuni hiyo, ilishindwa kulipa wafanyakazi wake kwa kile ilitaja kama kulemewa na athari za Covid – 19.
Kampuni hiyo Alhamisi imesema imefanya uamuzi huo baada ya kufanya mkutano wa mashauriano na Kamati ya Usimamizi wa Wafanyakazi na Muungano wa Kudheiha, ndio Kenya Union of Domestic, Hotels, Educational Institutions, Hospitals and Allied Workers mnamo Jumatano.
“Tunasisitiza wamiliki wa Mikahawa ya Fairmont wanajali maslahi ya wafanyakazi wake. Usimamizi umefutilia mbali notisi ya kufuta wafanyakazi, huku tukiendelea kufanya mashauriano na wadau husika hadi tuafikiane,” sehemu ya notisi mpya ya Fairmont inaeleza.
Uamuzi wa kubatilisha kufuta wafanyakazi wake unajiri siku kadhaa baada ya Wakili Mkuu wa Serikali Kennedy Ogeto kuandikia kampuni hiyo barua akitaka kuelezwa bayana sababu za kuwafuta.
Ikikashifu Fairment, Kudheiha ilitaja hatua ya kuwafuta kama ya “kulazimisha na inayokiuka mkataba uliopo wa makubaliano, CBA”.
Katika mkutano wa Jumatano, Muungano huo ulishinikiza wafanyakazi walipwe asilimia 50 ya mshahara wa mwezi Mei. “Tunashangaa kuona hatua zilizofuatwa na Usimamizi wa Fairmont zinakiuka CBA iliyoko kati yake na wafanyakazi,” Kudheiha inaeleza.
Janga la Covid – 19, ambalo sasa ni la kimataifa limeathiri uchukuzi na sekta zote kwa kiasi.