• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 6:27 PM
JAMVI: Mudavadi ageuza mbinu, akumbatia Raila na kuchanganya wafuasi

JAMVI: Mudavadi ageuza mbinu, akumbatia Raila na kuchanganya wafuasi

Na LEONARD ONYANGO

KINARA wa chama cha Amani National Congress (ANC) sasa amemkumbatia tena kiongozi wa ODM Raila Odinga baada ya juhudi zake za kutaka kujitenga na kuunganisha jamii ya Waluhya kuonekana kugonga mwamba.

Bw Mudavadi sasa anasema alitofautiana na Bw Odinga kuhusiana na masuala madogo madogo lakini hawajatalakiana kisiasa.

Bw Mudavadi na Bw Odinga walikutana kwenye jukwaa moja katika eneobunge la Shinyalu, Kaunti ya Kakamega wakati wa mazishi ya mamake mbunge wa eneo hilo Justus Kizito, ambapo wote walisisitiza kuwa bado wangali ndani ya NASA.

Bw Mudavadi alisema vinara wa NASA wangali pamoja kwani hakuna ambaye amewasilisha barua ya kutaka kujiondoa.

“Namheshimu Bw Raila na hatuna uadui baina yetu. Raila si mtu wa kupuuza hivi hivi,” akasema Bw Mudavadi.

Bw Mudavadi pia aliunga mkono pendekezo la kutaka Katiba ifanyiwe mabadiliko ambalo limekuwa likishinikizwa na Bw Odinga pamoja na viongozi wa ODM.

Uhusiano wa vinara wa NASA, Bw Odinga, Bw Mudavadi, Kalonzo Musyoka (Wiper) na Moses Wetang’ula (Ford-Kenya) ulitumbukia nyongo baada ya kinara wa ODM kukutana na Rais Uhuru Kenyatta mnamo Machi 9, mwaka huu.

Bw Odinga alikubali kushirikiana na Rais Kenyatta kutokana na kile alichokitaja kama juhudi za kutaka kuunganisha nchi. Bw Musyoka, Bw Mudavadi na Seneta wa Bungoma Wetang’ula walimtaja Bw Odinga kama msaliti.

Bw Wetang’ula amekuwa akimtaka Bw Odinga kugura NASA kwa misingi kwamba tayari amejiunga na serikali.

Bw Odinga amekuwa akisisitiza kuwa aliamua kushirikiana na Jubilee kwa lengo la kuhakikisha mabadiliko ambayo Upinzani umekuwa ukipigania yanatekelezwa.

Waziri huyo Mkuu wa zamani alisema yuko tayari kuunga mkono mmoja wa vinara wa NASA 2022 baada ya mageuzi kufanywa.

Kiongozi wa ANC Bw Mudavadi na Bw Wetang’ula waliafikiana kuvunjilia mbali vyama vyao na kuanzisha kampeni ya kuunganisha jamii ya Waluhya.

Hata hivyo, juhudi za Bw Mudavadi na Bw Wetang’ula kutaka kuunganisha jamii ya Waluhya zimeonekana kugonga mwamba baada ya viongozi kutoka maeneo ya Magharibi kujitenga na wawili hao.

Miongoni mwa viongozi ambao wamejitenga na wawili hao ni Waziri wa Ugatuzi Eugene Wamalwa, magavana Wycliffe Oparanya (Kakamega), Sospeter Ojaamong (Busia) na Seneta wa Kakamega Cleophas Malala kati ya wengine wengi.

Viongozi wanaopinga kampeni yao wanasema Bw Mudavadi na Bw Wetang’ula hawajafanya maendeleo yoyote katika ukanda wa Magharibi, hivyo hawana ushawishi wa kuunganisha jamii ya Waluhya.

 

Kujiokoa kisiasa

Bw Mudavadi amekuwa akishinikizwa kukumbatia Bw Odinga ili kujinusuru kisiasa.

Viongozi wa hivi punde kumshauri Bw Mudavadi kushirikiana na Bw Odinga ni wabunge Antony Oluoch (Mathare) na George Aladwa (Makadara) na Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna. Viongozi hao walimtaka Bw Mudavadi kushirikiana na Bw Odinga ikiwa anataka ndoto yake ya kuwa rais 2022 kutimia.

“Bw Mudavadi alikuwa amefanya makosa makubwa kwa kuendesha kampeni dhidi ya Bw Odinga katika maeneo ya Magharibi ambapo bado Waziri Mkuu wa zamani ana uungwaji mkubwa,” anasema Profesa Makau Mutua.

Kulingana na Prof Mutua, Bw Mudavadi anaweza kunufaika zaidi iwapo atashirikiana kwa karibu na Bw Odinga.

“Ikiwa Bw Odinga ataungana na Rais Kenyatta 2022, basi uwezekano wa Bw Mudavadi kunufaika na muungano huo ni mkubwa ikilinganishwa na endapo atajaribu kujitenga,” akasema Prof Mutua.

“Bw Mudavadi anakubalika katika maeneo ya Kati na hata Bonde la Ufa hivyo ni rahisi kwa Bw Odinga kumtetea kuungwa mkono au kuwa mwaniaji mwenza,” anaongezea.

Naye Seneta wa Elgeyo-Marakwet Kipchumba Murkomen anasema vita dhidi ya Bw Odinga vilitishia siasa ya Bw Mudavadi.

“Uwezekano wa Bw Odinga kuwania 2022 ni mfinyu mno, na ikiwa hatawania inamaanisha kuwa ataunga mkono mmoja wa vinara wenzake. Hivyo kujenga naye uaduni ni sawa na kujitia kitanzi cha kisiasa,” anasema Bw Murkomen.

You can share this post!

KINAYA: ‘Wiper’ ajue ufalme si moto wa sigara kupeanwa,...

JAMVI: Wito wa kurekebisha Katiba wazua uhasama wa mbio za...

adminleo