Uhuru alivyomtoa Ruto pumzi
BENSON MATHEKA Na WANDERI KAMAU
AMRI ya Rais Uhuru Kenyatta ya kuweka ofisi ya Naibu Rais chini ya ofisi yake ni mbinu ya kumpokonya Dkt William Ruto mamlaka na ushawishi wake serikalini, wadadisi wamesema.
Katika amri aliyotoa Jumatano alipopanga upya serikali yake, Rais Kenyatta alifanya ofisi ya Naibu Rais kuwa idara chini ya ofisi yake, akaipokonya pesa ilizokuwa ikitengewa katika bajeti na kumnyima nguvu za kuajiri wafanyakazi wake binafsi.
Hatua hii imejiri wakati ambapo Rais ameendelea kuwapokonya mamlaka bungeni viongozi ambao wanaegemea kwa naibu huyo, hata baada ya wawili hao kuonekana pamoja Siku ya Madaraka na kuchangamsha hasa wafuasi wa Dkt Ruto, wakidhania kuwa wameridhiana.
Wadadisi wa siasa wanasema hili ni pigo kubwa kwa Dkt Ruto na azma yake ya kugombea urais mwaka wa 2022 ikiwa atabaki katika chama cha Jubilee.
Kulingana na mdadisi wa siasa, Bw Javas Bigambo, ingawa agizo hilo halijaathiri majukumu ya Naibu Rais kikatiba, yamepunguza baadhi ya mamlaka ya afisi yake.
Anasema kuwa kinyume na awali, Dkt Ruto sasa atategemea Tume ya Kuwaajiri Wafanyakazi wa Umma (PSC) kuwaajiri wafanyakazi wa afisi yake.
Athari nyingine kwa Dkt Ruto ni kuwa afisi yake itapunguziwa bajeti iliyokuwa ikitengewa ili kuendesha majukumu yake.
“Mageuzi haya bila shaka yanamaanisha kuwa Dkt Ruto ni kama afisa wa kawaida wa serikali asiye na mamlaka yoyote. Mawaziri kwa sasa wanajishughulisha na utekelezaji wa ajenda ya Rais. Taswira iliyopo ni kuwa ataonekana tu kama walivyokuwa makamu wa rais wa hapo awali, ambapo waliteuliwa na Rais,” akasema.
Kwa kipindi cha miaka minane iliyopita, Dkt Ruto amekuwa akitumia ushawishi wa ofisi hiyo kujipigia debe, jambo ambalo halikumfurahisha Rais Kenyatta na wandani wake wakimlaumu kwa kumhujumu kiongozi wa nchi.
Wadadisi wanasema amri ya Jumatano ni sehemu ya hatua za kufifisha ushawishi wa Dkt Ruto ambaye alionekana maarufu katika chama cha Jubilee na serikalini akitumia mamlaka ya ofisi yake.
“Kwa Sasa, Dkt Ruto amenyang’anywa mamlaka ya mwisho aliyokuwa amebaki nayo mbali na majukumu yake ya kikatiba. Ni kumaanisha ushawishi wake utafifia kwa sababu atakuwa akiamuliwa mambo yake,” asema.
Kutolewa kwa amri hiyo kulijri huku Rais Kenyatta akiendelea kuwabandua wandani wa Dkt Ruto katika uongozi wa bunge na seneti. Wadadisi wanasema Rais alianza kwa kukata ‘kucha’ za Dkt Ruto katika chama tawala cha Jubilee.
Rais aliwaondoa wandani wa Ruto katika Kamati ya Kitaifa ya Usimamizi (NMC) ya chama hicho, hatua ambayo wandani wa Dkt Ruto walipinga. Kwenye mchujo wa uchaguzi mkuu wa mwaka jana, Dkt Ruto aliweka vibaraka wake katika ofisi muhimu za chama cha Jubilee ili aweze kukidhibiti. Mabadiliko ya kamati ya kitaifa ya usimamizi wa chama tawala, yalifuatiwa na Rais Kenyatta kuweka mkataba wa ushirikiano na chama cha Kanu bila kumhusisha Dkt Ruto.
Kulinga na na wadadisi, hatua hii ililenga kuongeza idadi ya wabunge na maseneta wanaomuunga Rais Kenyatta katika juhudi za kupunguza ushawishi wa Dkt Ruto.
Kabla ya Rais Kenyatta kuchukua hatua hiyo, wandani wa Dkt Ruto walikuwa wakijigamba kwamba ndio wengi katika chama na bungeni. Prof Macharia Munene, ambaye ni mchanganuzi wa siasa alisema kuwa lengo kuu la Rais Kenyatta ni kulainisha utendakazi wa serikali.
“Kile ambacho Rais Kenyatta amefanya ni kudhihirisha mamlaka yake, japo kwa msingi wa kikatiba, ” alisema.
Ushirikiano wa Jubilee na Kanu ulipisha kutimuliwa kwa wandani wa Dkt Ruto katika uongozi wa seneti kabla ya adhabu hiyo kuelekezwa katika bunge la kitaifa.
Miongoni mwa walioangukiwa na shoka ni Kipchumba Murkomen ambaye alikuwa Kiongozi wa Wengi katika seneti, Susan Kihika ambaye alikuwa Kiranja wa Wengi na Prof Kithure Kindiki aliyekuwa Naibu Spika.
Katika bunge la kitaifa, Bw Benjamin Washiali alipokonywa wadhifa wa Kiranja wa Wengi naye Cecily Mbarire akatemwa kama Naibu Kiranja.
Katika kile kinachoonyesha kuwa mikakati ya Rais imemtoa pumzi Dkt Ruto, hajajitokeza kuwatetea wandani wake wanaoadhibiwa kwa kumuunga mkono.
Vigogo wa kisiasa kutoka maeneo tofauti nchini wamekuwa wakimkwepa huku baadhi ya wabunge waliokuwa wakihusishwa naye wakitangaza uaminifu wao kwa Rais Kenyatta.