• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Waendeshaji bodaboda na tuktuk Ganjoni wapewa sanitaiza

Waendeshaji bodaboda na tuktuk Ganjoni wapewa sanitaiza

Na MISHI GONGO

WAHUDUMU wa bodaboda na Tuktuk wamenufaika na sanitaiza kutoka kwa serikali katika mpango wa kuzuia maambukizi zaidi ya ugonjwa wa Covid-19.

Akizungumza na wanahabari Ijumaa wakati wa kupeana sanitaiza hizo, chifu wa Ganjoni Mohammed Sadik alisema serikali inalenga sekta ya usafiri kwa sababu wahudumu hao kutangamana na watu wengi kila siku.

Chifu huyo alisema sanitaiza hizo zitawakinga wahudumu wa vyombo hivyo vya usafiri, familia zao pamoja na wateja wao.

Akishirikiana na mmiliki wa hoteli moja eneo la Ganjoni, Mama Jawambe, chifu huyo alimpongeza kwa kuwa mstari wa mbele katika kutafuta viyeyuzi kwa watu wa mashinani.

Chifu Sadik alisema mpango huo utaendelea hadi pale serikali itakapotangaza kuwa nchi iko salama na kwamba ugonjwa huo hatari si tisho kwa raia.

Mama Jawambe alisema ataendelea kukusanya vifaa zaidi vya kujikinga ili kuepuka virusi hivyo hatari ili kuwasaidia watu wa mashinani.

Msemaji wa wahudumu wa tuktuk eneo la Pwani Bw John Gatimu, aliishukuru serikali kwa hatua hiyo akisema kuwa wahudumu wengi hawana uwezo wa kununua sanitaiza.

Alisema kuwapa bidhaa hiyo kutawasaidia kukinga hali zao za kiafya.

Msemaji huyo aliiomba serikali kutoa sanitaiza zaidi kwa sababu sekta hiyo ina wafanyakazi wengi.

Wakati huo huo Bw Gatimu aliitaka serikali kuwaruhusu kubeba abiria wawili katika tuktuk ili kuwapunguzia hasara ambazo wanaendelea kukadiria tangu kuamrishwa kubeba abiria mmoja kwa kila safari.

You can share this post!

Kulegeza masharti kutasabisha vifo vingi – Uhuru

Ajabu ya mazishi kuhudhuriwa na watu 400 katika eneobunge...

adminleo