• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Uhuru anavyopimia Wakenya hewa

Uhuru anavyopimia Wakenya hewa

BENSON MATHEKA na VALENTINE OBARA

MATUMAINI ya Wakenya wengi kurejelea hali ya kawaida ya maisha kuanzia leo, yalizimwa jana wakati Rais Uhuru Kenyatta alipotangaza kuwa bado Kenya haina uwezo wa ‘kujihatarisha’ kwa mkurupuko zaidi wa virusi vya corona.

Rais alisema alichukua hatua hiyo kwa sababu juhudi za kuboresha hospitali ili zipambane na ugonjwa wa Covid-19 hazijafanikiwa kikamilifu kitaifa.

Pia alitaja idadi ya maambukizi inayoendelea kuongezeka, na uwezo mdogo wa kutafuta wanaotangamana na wagonjwa kama sababu za kutolegeza masharti upesi.

Ilifichuka kuwa viongozi wakuu na wataalamu wanaohusika kufanya maamuzi kuhusu mikakati ya kupambana na janga la corona hawakuelewana, kwani kulikuwa na waliotaka shughuli za kawaida zirejelewe huku wengine wakipinga.

“Baadhi yetu, mimi nikiwemo, tulitaka shughuli zifunguliwe hivi sasa. Bado hilo ni tamanio langu. Ninataka tufungue haraka iwezekanavyo ili tuendeleze uchumi,” akasema Rais.

Lakini, akasema, kwa kuzingatia hatari inayokodolea macho taifa hili endapo shughuli za kawaida zintarejelewa wakati huu, iliamuliwa masharti machache pekee yaondolewe na mengine yaendelee kudumu.

“Ni mjinga ambaye hasikilizi wataalamu wake. Wataalamu wetu wametambua kufungua nchi ni kuhatarisha maisha ya Wakenya. Tukifungua tukifikiria kuwa tunasaidia uchumi, mwishowe tutakuwa tumeharibu uchumi huo huo,” akaeleza.

Jana idadi ya maambukizi ya virusi vya corona ilipanda hadi 2,600 baada ya watu 126 kupatikana kuambukizwa. Wagonjwa wengine wanne walifariki, na kufikisha idadi kuwa 83.

Rais Kenyatta aliagiza Wizara ya Elimu na ile ya Afya kuweka mikakati ya kuanza kufungua shule kuanzia Septemba. Inatarajiwa shule zitafunguliwa kwa zamu, nayo ratiba ya masomo itatolewa Agosti.

Ijapokuwa makanisa yataendelea kufungwa, kuna matumaini kwani Rais aliagiza Wizara ya Usalama na ile ya Afya kuunda baraza la viongozi wa dini katika muda wa siku saba, ili litoe mwongozo kuhusu jinsi ambavyo ibada zitaendelezwa huku vita vya corona vikiendelea.

Marufuku ya kutotoka nje usiku itaendelea kwa siku 30 zaidi. Hata hivyo, kuanzia leo, kafyu itakuwa kati ya saa tatu usiku hadi saa kumi alfajiri badala ya saa moja usiku hadi saa kumi na moja alfajiri ilivyokuwa.

Rais Kenyatta alisema hii itawezesha wananchi kuendelea na kazi zao bila wasiwasi wa kuvunja sheria.

Jijini Nairobi, kumekuwa na misongamano ya magari baada ya saa moja usiku kwa wiki kadhaa sasa.

Rais pia aliongeza muda wa kutoingia na kutoka Nairobi, Mombasa na Mandera kwa siku 30, akazima matumaini ya wengi walionuia kusafiri maeneo ya mashambani. Kaunti za Kwale na Kilifi zilipata afueni kwani watu wataruhusiwa kuingia na kuondoka kuanzia leo, sawa na mitaa ya Eastleigh (Nairobi) na Old Town (Mombasa).

“Kilifi na Kwale maambukizi yameanza kupungua kwa hivyo tunaanza kufungua. Hapa Nairobi ugonjwa unaenda juu ndiposa tunasema Nairobi si kama Kwale na Kilifi. Tumefungua kule ambapo ugonjwa umeanza kuteremka na tumeendelea kufunga pale ambapo ugonjwa unaenda juu. Hatutaki kueneza ugonjwa kwa kaunti nyingine,” akasema.

Mkutano utakaojumuisha magavana wote na viongozi wa serikali kuu utafanywa Jumatano ili kila kaunti itoe hakikisho kuwa itaweka mikakati ya kutosha dhidi ya virusi vya corona.

Rais aliongeza marufuku ya mikutano ya hadhara ya aina yoyote ikiwemo sehemu za burudani kwa siku 30. Hii inamaanisha Wakenya hawatakuwa na uhuru wa kuhudhuria mazishi na harusi katika muda wa siku 30 zaidi.

Safari za kuingia na kutoka nchini pia zingali zimepigwa marufuku kwa muda usiojulikana.

You can share this post!

Arsenal yaadhibu Charlton 6-0 Nketiah akifuma matatu

Abambwa baada ya kumuua mwanawe

adminleo