• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Wizara yataka itengewe Sh20 bilioni kukarabati barabara

Wizara yataka itengewe Sh20 bilioni kukarabati barabara

Na WALTER MENYA

WIZARA ya Barabara na Miundomsingi inataka bunge na Wizara ya Fedha kutenga karibu Sh20 bilioni za dharura ili kukarabati barabara zilizoharibiwa na mvua inayoendelea kunyesha nchini.

Huku Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa ikisema mvua itaendelea kunyesha hadi katikati ya Mei, huenda gharama ya kukarabati barabara zilizoharibiwa ikapanda zaidi.

Kulingana na barua iliyoonekana na Taifa Leo, Katibu katika wizara hiyo, Bw Julius Korir alisema wameomba Wizara ya Fedha kutenga Sh2 bilioni “kutuwezesha kuchukua hatua kwa dharura katika ujenzi wa barabara na kurudisha hali ya kawaida barabarani”.

Wizara hiyo pia inataka bunge liidhinishe Sh17.5 bilioni ambazo zitagawanywa kwa mashirika matatu ya barabara nchini, ambazo ni Mamlaka ya Barabara Kuu za Kenya (KeNHA), Mamlaka ya Barabara za Miji ya Kenya (KURA) na Mamlaka ya Barabara za Mashambani Kenya (KeRRA).

Kiwango hiki cha fedha huenda kimebadilika kwa sababu mvua kubwa inayonyesha pembe tofauti za Kenya imebomoa barabara kadhaa na kufanya zingine zifurike.

“Kutokana na mvua kubwa inayonyesha nchini, mafuriko yamesababisha uharibifu mkubwa kwa miundomsingi ya barabara,” akasema Bw Korir, kwenye ripoti fupi kuhusu hali ya barabara za nchi.

Imependekezwa KeNHA ipewe Sh2.5 bilioni, KeRRA Sh11 bilioni na KURA Sh4 bilioni.

Katibu huyo alisema pesa hizo zinahitajika kwa sababu wizara imemaliza pesa zilizotengewa mambo ya dharura “na kwa hivyo tumelemewa katika kuchukua hatua ipasavyo wakati kunapotokea mahitaji ya dharura”.

Barabara za mashambani zilizoharibika zaidi ni katika Kaunti za Turkana, Wajir, Makueni, Machakos, Narok, Mandera, Garissa, Busia, Kisumu na Tana River.

You can share this post!

Miguna apinga vikali juhudi za kubadili katiba

KFS lawamani kulemewa kuimarisha huduma za feri Mtongwe

adminleo