Habari Mseto

Seneta ataka Mudavadi ampigie debe Ruto aingie Ikulu 2022

April 30th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na TITUS OMINDE

SENETA wa kaunti ya Nandi Bw Samson Cherargei (pichani)ametaka kinara wa chama cha ANC Musalia Mudavadi kujitoa kwenye muungano wa Nasa na kujiunga na naibu rais William Ruto ampigie debe mwaka wa 2022.

Akihutubu wakati wa sherehe ya kushukuru Mungu kwa kuchaguliwa kwa mbunge wa Sabatia, Bw Alfred Agoi katika uwanja wa shule ya upili ya Chavakali, Bw Cherargei alisema iwapo Mudavadi atamuunga mkono Ruto atapata wadhifa mkubwa serikalini Ruto akichaguliwa rais 2022.

“Sisi ni majirani wenu hapa. Iwapo jamii ya Waluhya ingependa kuwa serikalini, basi Mudavadi hana budi kuongoza jamii hii kumpigia debe Ruto mwaka wa 2022,” akasema Bw Cherarget.

Seneta huyo alisema licha ya rais Uhuru Kenyatta kutaka mjadala wa 2022 kusitishwa alitilia mkazo kuwa kama Jubilee wameshaamua hakuna mtu ambaye atapinga Ruto katika chama hicho mwaka wa 2022 katika wadhifa wa rais.

“Sioni kujipanga kwenye nyinyi kama jamii ya Waluhya mnajipanga tayari sisi tumejipanga Mudavadi anapaswa kuachana na mtu wa vitendawili ili alete jamii ya Waluhya pamoja serikalini kwa kuunga mkono naibu rais” alisema Bw Cherargei.

Hata hivyo Mudavadi alitupilia mbali tetesi hizo na kusema kuwa yuko imara katika Nasa, huku akitaka jamii zote nchini kuunga mkono mgombezi wa kiti cha urais kutoka katika muungano huo kwa uongozi mwema nchini ifikapo 2022.