• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 12:48 PM
Walimu mjini Mombasa washtaki shule kwa kuwakata asilimia 65 ya mshahara

Walimu mjini Mombasa washtaki shule kwa kuwakata asilimia 65 ya mshahara

Na BRIAN OCHARO

WALIMU wanane kutoka shule ya mmiliki binafsi ya Jaffery mjini Mombasa wameishtaki kwa kuwakata asilimia 65 ya mshahara wao bila kuwaomba idhini.

Walimu hao Bw Emanuel Wambua, Erick Solonic, Boniface Lwova, Richard Onyango, Edwin Gisemba, Edward Ogugi, Alpha Mwanyika na Bi Rosemary Rarieya wanashtumu usimamizi wa shule kwa kuwabagua baadhi ya walimu.

Katika stakabadhi waliyowasilisha katika mahakama ya kushughulikia maswala ya wafanyakazi mjini humo, wanasema mbali na kuenda kinyume na makubaliano ya ajira, pia wasimamizi waliwatoa katika orodha ya walimu watakaopeana mafunzo mitandaoni.

“Hatukuwa na majadiliano ya aina yoyote na usimamizi wa shule; tunahisi kuonewa. Hali hiyo pia imetufanya kukumbwa na msongo wa mawazo,” inasema sehemu ya stakabadhi hiyo.

Wanaongeza kwamba usimamizi huo haukusema hali hiyo itadumu kwa muda gani, hivyo kuwafanya kupitia hali ngumu ya kiuchumi kufuatia mshahara mdogo wanaoupata.

“Tuna mikopo ambayo tunalazimika kulipa hivyo baada ya kukatwa, pesa tunazopokea ni chache mno na haziwezi kukidhi mahitaji yetu,” inasema stakabadhi yao.

Wanaeleza kuwa bodi ya shule hiyo haikuweka wazi iwapo pesa walizokatwa zitalipwa baada ya kuisha kwa janga la corona au la.

Walimu hao aidha wametaka mahakama iamuru shule hiyo kuwalipa fidia kwa kukiuka haki zao za ajira.

Wanasema shida ilianza mwezi Aprili; siku chache baada ya Rais Uhuru Kenyatta kutangaza kufungwa kwa shule zote nchini kama njia mojawapo ya kudhibiti kuenea kwa virusi vya corona.

Baada ya uamuzi wa kufungwa shule, usimamizi ulikubaliana kuwa walimu wote wafundishwe kusomesha watoto kupitia mitandao.

Wanaeleza kwamba mafunzo yaliendelea kwa muda wa wiki mbili kabla ya shule kufungwa. Muda huu wote walidai kuwa shule hiyo haikuwapa vifurushi vya data wala tarakilishi za kufanyia mafunzo hayo.

“Mapenzi kwa kazi yetu na wanafunzi yalitufanya tukagharimika kununua vifaa vilivyohitajika kutekeleza mafunzo ya mtandaoni. Hata hivyo, baadaye usimamizi wa shule uliwalazimisha walimu wote kwenda mapumziko ya lazima ya siku 21,” inasema sehemu ya nakala hiyo.

Walimu wote walihimizwa kufanya mazoezi ya kutumia mitandao na pia kutayarisha mijarabu ya wanafunzi.

Hata hivyo baada ya shule kufunguliwa – mtandaoni – baadhi ya walimu walitolewa katika orodha ya kufundisha.

Juhudi zao za kuzungumza na usimamizi wa shule hiyo hazikufua dafu na baadaye waliorodheshwa kuwa walimu wasiotoa huduma muhimu na kuarifiwa kuwa watakatwa asilimia 65 ya mshahara huku walioorodheshwa kufunza kupitia mitandao wakiambiwa kuwa watakatwa asilimia 45.

You can share this post!

SIHA NA LISHE: Ukitaka protini kula vyakula hivi

Safaricom yafunga maduka manne kuyanyunyuzia dawa

adminleo