• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 4:48 PM
Safaricom yafunga maduka manne kuyanyunyuzia dawa

Safaricom yafunga maduka manne kuyanyunyuzia dawa

Na WINNIE ATIENO

KAMPUNI ya Safaricom imefunga maduka yake manne kwa muda wa siku mbili ili kuyanyunyuzia dawa kama hatua mojawapo ya kuepushia wafanyakazi na wateja hatari ya virusi vya corona.

Maduka hayo ni lililo eneo la Nyali na lile la Rex House ambapo haya mawili ni ya mjini Mombasa, lile la Thika na lile la Lavington Mall yamefungwa hii leo Jumanne hadi Juni 11 watakapomaliza shughuli hiyo.

Aidha kampuni hiyo imetangaza kwamba itakuwa ikiendeleza shughuli hiyo ya unyunyuziaji wa dawa mara kwa mara.

“Kama tujuavo ulimwengu unaendelea kupambana na virusi vya corona. Safaricom itaendelea kuchukua hatua madhubuti za kupambana na kuzuia maambukizi ya virusi hivi ili kuhakikisha afya na usalama wa wafanyakazi na wateja wetu,” Afisa Mkuu Mtendaji wa Safaricom Bw Peter Ndegwa alisema.

Kwenye taarifa iliyochapishwa na Safaricom na kusambazwa kupitia akaunti yake ya Twitter kampuni hiyo ya mawasiliano imesema itakuwa inafanya shughuli hiyo mara kwa mara.

“Jukumu letu kuu ni kuhakikisha usalama wa wafanyakazi na wateja wetu huku tukiendeleza shughuli za kusaidia serikali katika kukabiliana na janga hilo, ”ameongeza Bw Ndegwa.

Hata hivyo kampuni hiyo imewaambia wateja wake waendelee kupata huduma kupitia mitandaoni na maduka mengine karibu na yale ambayo yamefungwa.

Hatua hiyo inajiri huku kaunti ya Mombasa ikiendelea kupata visa zaidi vya wagonjwa wa Covid-19.

Leo Jumanne Waziri Msaidizi wa Afya ametangaza visa 34 vya Mombasa kati ya jumla ya visa vipya 127.

Idadi jumla ya visa vya Covid-19 nchini vimefika 2,989 na hivyo ipo haja ya watu kuchukua tahadhari.

You can share this post!

Walimu mjini Mombasa washtaki shule kwa kuwakata asilimia...

Jengo laporomoka mjini Kericho

adminleo