Habari

Viongozi wanawake wamtetea Waiguru

June 10th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

CHARLES WASONGA na SAMMY WAWERU

VIONGOZI wanawake wamemtetea Gavana Anne Waiguru saa chache baada ya hoja ya kumwondoa afisini kupitishwa katika Bunge la Kaunti ya Kirinyaga.

Waziri wa Utumishi wa Umma na Masuala ya Kijinsia na Mbunge Mwakilishi wa Wanawake wa Homa Bay Gladys Wanga wamedai kuwa hatua hiyo haifai kwani inalenga kudumaza uongozi wa wanawake nchini

Prof Kobia amelaani madiwani wa Kirinyaga waliopitisha hoja ya kumwondoa afisi Gavana Waiguru hawathamini uongozi wa wanawake.

Mnamo Jumanne madiwani 23 kati ya 33 walipitisha hoja hiyo, licha ya kuwepo kwa amri ya mahakama ya kuzuia kujadiliwa kwake, na sasa uamuzi huo unasubiriwa kuwasilisha kwa Seneti baada ya siku tatu.

“Muhula wa uongozi wa Gavana Waiguru unakatizwa na kura hiyo ambayo haikuwasilishwa kwa njia halali. Hii ina maana kuwa kuna watu ambao hawathamini uongozi madhubuti wa wanawake,” Profesa Kobia akasema kwenye taarifa.

“Inavunja moyo kwamba Gavana huyo anaondolewa mamlakani katika kipindi hiki cha vita dhidi ya Covid-19, ambayo imeathirika pakubwa maendeleo katika nyanja zote nchini,” taarifa hiyo ikaongeza.

Naye Bi Wanga akasema kupitia ujumbe katika akaunti yake ya Twitter: “Hoja hiyo ilidhaminiwa na baadhi ya viongozi ambao wanauenea wivu utendakazi mzuri wa Bi Waiguru kwa sababu yeye ni mwanamke,”

“Bunge la Seneti inapasa kutupilia mbali uamuzi huo kwa sababu ulifikia kutokana na sababu zisizo na mashiko,” akaongeza Bi Wanga.

Mbunge huyo, ambaye alisema yeye ni mtetezi sugu wa Ajenda ya Wanawake Nchini Kenya (COWA) aliongeza kuwa utaratibu wa kisheria haukufuatwa wakati wa kujadiliwa na kupitishwa kwa hoja hiyo.

Mwingine ni Gavana wa Kaunti ya Kitui Charity Ngilu ambaye amemfariji na kumtaka awe ngangari katika kuhudumia wakazi wa Kirinyaga.

“Ni miongoni mwa njia zisizo halali zilizotumiwa na mitandao ya kumuondoa madarakani, tunakashifu hayo,” Gavana Ngilu amechapisha katika ukurasa wake wa Twitter na Facebook.

 

Spika wa bunge la kaunti ya Kirinyaga Antony Gathumbi anatarajiwa kuwasilisha mapendekezo ya bunge hilo kumbandua Waiguru kwa spika wa seneti Ken Lusaka, ambapo seneti itajadili mswada huo na kutoa uamuzi.

Endapo seneti itaridhishwa na hoja za bunge la kaunti ya Kirinyaga kumuondoa afisini, Waiguru anaweza kuelekea mahakamani kukata rufaa.

Lakini Rais wa Chama cha Mawakili Nchini (LSK) Nelso Havi alipuuzilia mbali kauli ya Waziri Kobia akisema Waiguru alichaguliwa baada ya ufaafu wake kukaguliwa sawasawa.

“Kama utetezi wake wa jinsia ya kike ni halali, basi awasilishe ombi kwa Jaji Mkuu David Maraga afutilie mbali bunge kwa kutotimiza hitaji la kikatiba kuhusu usawa wa kijinsia,” akasema Bw Havi kupitia Twitter.

Mnamo Jumanne madiwani 23 waliopiga kura ya kumwondoa afisini Gavana Waiguru kwa misingi ya mienendo mibaya na matumizi mabaya ya afisi

Hoja hiyo iliwasilishwa na Diwani wa Wadi ya Mutira David Kinyua Wangui. Madiwani wanne walisusia upigaji kura na wengine sita hawakuhudhuria kikao hicho cha bunge la Kaunti ya Kirinyaga.

Mapema vurugu zilizuka katika bunge hilo baada ya madiwani Athony Munene (wa wadi ya Karumandi) na diwani maalum Lucy Njeri, ambao ni wandani wa Waiguru, kufurushwa kutoka ukumbini.

Waiguru ametoa taarifa akilaani hatua ya madiwani waliopitisha hoja hiyo aliyoitaja kama inayokwenda kinyume na sheria “kwa kujadiliwa licha ya mahakama kutoa amri kwamba isitishwe.”