TAHARIRI: Mvutano wa Rais na Maraga haufai
Na MHARIRI
KWA kipindi cha majuma mawili sasa, nchi ya Kenya imegeuzwa kuwa uwanja wa kumenyana kwa mafahali wawili wakuu.
Tatizo ni kwamba sawa na walivyosema wazee wetu, mafahali wapiganapo ni nyasi ndizo huumia.
Kwa mujibu wa Katiba ya Kenya, mfumo wa utawala una ngazi tatu: Kitengo cha Urais, Bunge na Mahakama. Waliotunga Katiba waliazimia kwamba ngazi hizi tatu zitafanya kazi kwa ushirikiano ili kukamilishana japo kila ngazi ina jukumu bainifu.
Kitengo cha Urais hutarajiwa kutekeleza maazimio ya Wakenya kupitia kwa mwongozo wa Katiba na sheria zitungwazo na Bunge. Bunge nalo kwa upande wake huwa na majukumu matatu makuu; kutunga sheria, kuwakilisha matakwa ya mwananchi na kufanya tathmini ya utendakazi wa Rais. Kwa upande mwingine, mahakama nayo huhakikisha kwamba Bunge linatunga sheria zinazowiana na matakwa ya Katiba na pia kuhakikisha kwamba kitengo cha Urais kinahudumia taifa kwa kufuata sheria.
Ukichunguza kwa makini majukumu yaliyoorodheshwa, kila kitengo kina kazi maalum na hivyo basi hutarajii kuwepo mkwaruzano wowote.
Katika malalamishi yake kwa rais siku ya Jumatatu, Jaji Mkuu David Maraga aliteta kwamba Serikali Kuu pamoja na ofisi ya Rais inakiuka mwongozo wa sheria na hivyo kuwa mfano mbaya kwa umma. Aliorodhesha visa kadha vya awali ambapo mahakama ilitoa maagizo ila serikali ikayakiuka. Mfano wa karibuni zaidi ni ubomozi wa makazi katika mtaa wa Kariobangi uliokuwa umesitishwa na mahakama.
Lililomkera Maraga hata zaidi ni hatua ya Rais Uhuru Kenyatta kukataa kuidhinisha orodha ya majaji 41 waliokuwa wamepigwa msasa na Tume ya Huduma za Mahakama (JSC). Mkwamo huu umekuwepo kwa zaidi ya mwaka mmoja.
Hata hivyo, Jumanne Mwanasheria Mkuu Paul Kariuki Kihara alijitokeza na kumjibu Maraga kuhusu madai ya siku ya Jumatatu. Katika utetezi wake, Kihara alimtaja Maraga kama mtu anayetafuta umaarufu kutoka kwa umma kwani mengi ya madai yake si ya kweli.
Alisisitiza kwamba Rais hatashinikizwa na yeyote kuidhinisha orodha ambayo ina baadhi ya majaji walio na doa.
Ubabe na mkwaruzano huu bila shaka haumsaidii kwa vyovyote mwananchi wa kawaida. Rais na jaji Maraga wanafaa kuandaa kikao cha kusuluhisha tofauti hizi faraghani ili kuepuka kujiumbua.