COVID-19: Wakazi wa maeneo duni Nakuru wanufaika na matangi ya maji ya kutiririka
Na PHYLLIS MUSASIA
ROTARY Club mjini Nakuru imeshirikiana na benki ya Stanbic kupeana bure matangi ya maji ya kutiririka kuwawezesha wakazi wa mitaa duni kunawa mikono mara kwa mara kama mojawapo ya njia za kuepuka maambukizi ya Covid-19.
Jumla ya matangi 30 yalipeanwa kwa mitaa ya Rhonda, Weavers na mtaa wa eneo la kutupa taka la Gioto ulioko Nakuru Magharibi.
Kulingana na mkurugenzi wa shughuli za Rotary Club Bi Ashley Gasperi, mradi huo wa kitaifa utafanyika katika mitaa yote duni nchini ili kuimarisha usafi na mazingira wakati huu wa janga la Covid-19.
Matangi yaliyosambazwa katika mitaa hiyo tatu yanatumia msimbo wa teknolojia ambapo iwapo maji yatapungua au sabuni kuisha, wakazi watakakiwa kutumia simu za kisasa kuwasilisha ujumbe na kisha maji au sabuni kuongezwa katika sehemu ambazo matangi hayo yatawekwa.
Bi Gasperi alisema njia ya teknolojia itarahisisha kazi baina ya wakazi na wahisani katika kipindi chote cha janga.
“Tuko katika vita hivi pamoja na kila mmoja wetu anapaswa kuwajibika pasipo na viwango vya maisha. Wakazi wa maeneo duni hupitia changamoto za rasilimali kama vile maji na sabuni na wakati huu, kila mmoja wetu anahitajika kuzingatia usafi wa hali ya juu ili kuepuka maambukizi,” akasema.
Meneja wa benki ya Stanbic tawi la Nakuru Bw Leonard Surmat alisema wakazi wengi wa mitaa ya mabanda wako katika hali ya hatari ya kuambukizwa virusi vya corona kutokana na hali ngumu ya maisha na mipangilio mibaya kimazingira.
Bw Surmat alisema asilimia kubwa ya watu wa viwango vya chini maishani huishi katika sehemu hizi wakiwemo wakongwe, wanawake, watoto na watu walemavu ambao wanapaswa kusaidiwa sana wakati huu.
Alieleza kwamba matangi hayo yatawasilishwa kwa watu watakao chaguliwa na viongozi wa wanyumba kumi pamoja na machifu ili kuimarisha usalama wake.
Kulingana naye, vyakula vya misaada na vitu vingine vya matumizi vinavyotolewa na wahisani wakati huu, vinapaswa kusambwa kwa wakazi wa mitaa duni bila ubaguzi kutoka kwa viongozi au wasimamizi wa mipango ya kupambanana na janga la Covid-19.
Mashirika hayo mawili yatashirikiana kuwafikia watu mbalimbali nchini wanaohitaji misaada.
Mzee wa mtaa wa Rhonda Bw Rajab Langoi alishukuru mashirika hayo mawili kwa msaada wa matangi hayo huku akisema kwamba yamewafikia wakazi kwa wakati ufaao.
“Tulihitaji sana vifaa hivi ili kutoa huduma kwa idadi kubwa ya wakazi kwa wakati mmoja. Watu wengi wa hapa wana shida ya maji kwa sababu yale wanayotumia kwa matumizi ya nyumbani ni ya kununua,” akasema.
Aliongeza kuwa wengi wao wamepoteza ajira na pesa wanazopata baada ya kufanya kazi ndogo ndogo, wao hununua vyakula na kisha kubaki katika hali ya sina sinani huku taswira nzima ikiwaweka katika hali hatari ya maambukizi.