Makala

TAHARIRI: Utendakazi ndio muhimu si jinsia

June 11th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na MHARIRI

HATUA ya madiwani wa Kaunti ya Kirinyaga kupitisha hoja ya kumng’oa mamlakani Gavana Anne Waiguru, iliibua mjadala mitandaoni Jumatano.

Mjadala ulioibuka ulihusiana na iwapo hatua imetokana kwa sababu ya jinsia yake ama utendakazi wake.

Ingawaje kila mmoja ana haki ya kutoa maoni yake, ni muhimu katika karne tuliyopo kuhakikisha kuwa tunatoa nafasi sawa kwa jinsia zote na wala sio kukandamiza yeyote kijinsia.

Jinsi miaka inavyokwenda, mtoto wa kike amedhihirisha kuwa licha ya jinsia yake kuonekana kuwa ya mtu dhaifu, ana uwezo wa kufanya mengi na kupaa sawa na wenzake wa kiume.

Lakini pia ni muhimu kwa kila mmoja kufahamu kuwa anastahili kuwajibikia majukumu ama nafasi aliyopewa, na msimamo unaochukuliwa dhidi ya mtoto wa kiume, usimbague wa kike.

Wanaume waliopo kwa nyadhifa mbali mbali, wanafaa kuwajibikia maamuzi na utendakazi wao sawa na wanawake.

Haitafaa kwa wanaume au wanawake kujitokeza kutetea jinsia yao wakati hawana ufahamu wa uzito wa masuala yanayomkabili mtuhumiwa yeyote.

Ni vyema kwa mshikamano kuwepo lakini pia ni bora kuelewa athari za kupinga hatua dhidi ya mtu anayetuhumiwa kwa ufisadi kwa sababu ni wa jinsia moja nawe,koo au kabila.

Nchini Kenya, suala la ukabila pia hujitokeza kila wakati ambapo mtu anayeshikilia wadhifa fulani anapokabiliwa na tuhuma mbalimbali.

Kwa hivyo, ni muhimu kuhakikisha kuwa masuala ambayo yanaathiri walipa ushuru ama wapiga kura ndiyo yanapewa uzito, hasa kunapokuwa na kesi za ufisadi. Itasikitisha ikiwa suala la jinsia au ukabila litatumika kutetea ama kuwaponda wanaokabiliwa na tuhuma tofauti.

Watu wa jinsia zote wanastahili kuelimishwa kuhusu umuhimu wao katika ujenzi wa taifa, kuthamini watu wa jinsia zote na kulenga kuwa na usawa, kwa kutoa nafasi sawa kwa wote.

Hali hii itaboresha maisha sio kwa Wakenya tu bali ulimwengu kwa jumla kwa kuangazia taasisi za elimu, ajira ulingo wa siasa miongoni mwa sekta nyingine.