Michezo

Mzaha wa Dele Alli kuhusu corona wampokeza adhabu kali

June 12th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHRIS ADUNGO

KIUNGO Dele Alli wa Tottenham Hotspur amepigwa marufuku ya mechi moja na Shirikisho la Soka la Uingereza (FA) kwa sababu ya ujumbe alioupakia kwenye mtandao wa kijamii kuhusiana na janga la corona.

Mnamo Februari, Alli, 24, alipakia kwenye Snapchat video aliyoitumia kufanyia mzaha mlipuko wa corona na kumdhihaki mwanamume mmoja mwenye asili ya Asia aliyekuwa ameathiriwa na virusi vya homa hiyo.

Nyota huyo mzawa wa Uingereza pia amepigwa faini ya Sh7 milioni na ameamriwa kushiriki kozi ya mafunzo kuhusiana na ugonjwa wa corona.

Marufuku ambayo Alli amepokezwa yamaanisha kwamba atakosa mechi ya nyumbani itakayowakutanisha sasa na Manchester United mnamo Juni 19.

Katika video iliyochukuliwa na Alli, kiungo huyo alionekana akiwa amevalia barakoa kwenye uwanja wa ndege, kabla ya kuelekeza kamera yake kwa mwanamume mwenye usuli wa Asia kisha kumulika chupa zilizokuwa na sanitaiza.

Katika kujitetea kwake, Alli alisema “alitambua haraka kwamba video hiyo ingezua hisia kali miongoni mwa waathiriwa” ndiposa akaifuta haraka haraka kabla ya kuabiri ndege.

Alli pia alisema kuwa alikuwa “amesalitiwa” na rafiki mmoja aliyeuza video hiyo iliyokuwa kwenye akaunti yake binafsi ya mtandao wa jamii kwa vyombo vya habari vilivyoiangazia na kuchangia kushtakiwa kwake.

Katika taarifa yake, Alli alisema: “Kufuatia maamuzi ya FA, ningependa kuomba msamaha kwa mara nyingine kuhusiana na hisia zilizoibuliwa na mienendo yangu. Ni mzaha ambao wakati nikiufanya, sikutarajia kuwa janga la corona lingeyumbisha dunia nzima kama tunavyoshuhudia kwa sasa.”

Kufikia sasa, zaidi ya watu 41,000 wameaga dunia kutokana na ugonjwa wa Covid-19 nchini Uingereza huku zaidi ya vifo 416,000 vikiripotiwa dunia nzima.