Habari

Yatani akiri alikabiliwa na kibarua kigumu kusawazisha bajeti

June 12th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

WAZIRI wa Fedha Ukur Yatani ameungama kuwa bajeti aliyowasilisha kwa Wakenya bungeni Alhamisi jioni ilitokana na maamuzi magumu ambayo yeye na maafisa wake walifikia kwa lengo la kuendeleza taifa hili wakati huu mgumu.

Akiongea na wanahabari muda mfupi baada ya kusoma bajeti ya mwaka wa kifedha wa 2020/2021, Yatani alipongeza wadau wote walioshiriki katika mchakato wa utayarishaji wa bajeti.

“Katika mazingira ya uhaba wa rasilimali huku changamoto kama vile Covid-19, mafuriko na uvamizi wa nzige zikiathiri uchumi, haikuwa kazi rahisi kuandaa bajeti inayoshirikisha vipengele vyote muhimu kwa usawa,” akasema, akiongeza ameisoma bajeti hii wakati maalum.

Kwa muda wa saa moja na dakika 40, Bw Yatani alisoma bajeti akiangazia masuala ya afya, usalama, ajenda nne za maendeleo za serikali, kati ya mengine muhimu kwa taifa hili.

Kwa mfano, Waziri alitenga Sh1.2 bilioni za kutumika kuajiri wahudumu 5,000 wa afya watakaopiga jeki vita dhidi ya janga la Covid-19.

Alisema wahudumu hao watafanya kazi chini ya kandarasi ya mwaka mmoja hasa katika maeneo ya mashinani yanayokabiliwa na uhaba mkubwa wa wahudumu hao.

Vilevile, alitenga Sh500 milioni kufadhili mpango wa ununuzi wa vitanda 20,000 vilivyotengenezwa humu nchini na vitakavyosambazwa katika hospitali za umma.

Na Sh25 milioni zimetengwa kupiga jeki mpango wa ujenzi wa mitambo ya kisasa ya sanitaiza katika vituo vya mipakani na hospitali kuu kote nchini.

Katika sekta ya Nyumba, serikali imetenga Sh15.5 bilioni kugharimia mpango wa ujenzi wa nyumba za gharama ya chini.

Vilevile, katika bajeti hii ambayo itaanza kutekelezwa kuanzia Julai 1, 2020, Waziri Yatani ametenga Sh3.6 bilioni kutoka Benki ya Maendeleo Afrika (ADB), Sh7.5 bilioni kutoka Mpango wa Ustawishaji Miji na Sh1.1 bilioni kugharimia ujenzi wa masoko katika maeneo ya Gikomba, Githuria, Chaka, Kamukunji na Githurai.

Na kuhusiana na mpango wa kufufua uchumi ulioathiriwa na janga la Covid-19, Bw Yatani alisema wizara yake itahakikisha kuwa Sh10 bilioni zilizotengwa kwa ajili ya mpango wa “Kazi Mitaani” zinawafaidi vijana wanaostahili.

“Serikali inalenga kuwafaidi zaidi ya vijana 200,000 katika mitaa ya miji mikubwa kama Nairobi, Mombasa, Kisumu, Nakuru, Eldoret, miongoni mwa mingine katika kaunti nane. Vijana hawa watakuwa wanazibua mitaro ya majitaka na kuzoa taka katika mitaa kadha,” akasema Bw Yatani.

Pesa hizo, Sh10 bilioni ni sehemu ya Sh53.8 ambazo serikali imetanga kwa ajili ya kufadhili mipango mbalimbali chini ya nguzo nane za kuchochea ufufuzi wa uchumi ulioyumbishwa na makali ya Covid-19.