Habari Mseto

Polisi 3 waliohusika kumvuta Mercy Cherono kwa pikipiki motoni

June 12th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

NA ERIC MATARA

Polisi watatu na raia mmoja waliohusika katika kitendo cha unyama dhidi ya mwanamke mmoja katika Kaunti ya Nakuru kwa kumfunga kwa pikipiki na kumvuta barabarani eneo la Olenguruone wamekamatwa.

Kukamatwa kwao kunajiri siku mojabaada ya umma kulilia haki ya mwanamke huyo aliyeumizwa vibaya usoni na tumboni.

Video ya mwanamke huyo kwa jina Mercy Cherono mwenye mika 21 akivutwa iliyosambaa mitaani ilizua hisia kali na hamaki  miongoni mwa wananchi, viongozi na wanaharakati wa haki za kibinadamu.

Mshirikishi wa eneo la Bonde la Ufa George Natembeya aliyetembelea mwanamke huyo katika hospitali kuu ya kaunti ya Nakuru alithibitisha kwamba polisi watatu na raia waliohusika na kitendo hicho wamekamatwa na wanendelea kuhojiwa na maafisa wa upelelezi kutoka kitengo cha DCI Nakuru.

“Tumewakamata polisi watatu na raia mmoja na wanendelea kuhojiwa ili kusaidia na uchunguzi zaidi. Tumeanzisha uchunguzi ili tujue nini kilipelekea kitendo hicho. Tukimaliza uchunguzi wale ambao watapatikana na hatia watafunguliwa mashtaka,” alisema Bw Natembeya.

Taifa Leo iligundua kwamba kati ya wanne hao waliokamatwa, mmoja wao ni naibu wa afisa mkuu wa kituo polisi cha Olenguruone ambaye ni mhusika mkuu katika kesi hiyo.

Mr Natembeya, aliyekuwa pamoja na kamanda wa polisi wa eneo hilo Marcus Ocholla walisema kwamba mwathiriwa alikuwa anaendelea kupona majeraha hospitalini.