Liverpoool wakubaliwa kuchezea mechi zao Anfield
Na CHRIS ADUNGO
MEYA wa Liverpool, Joe Anderson, amepiga abautani na kuwakubalia Liverpool kuchezea mechi zao zilizosalia za nyumbani ugani Anfield na kuidhinisha pia gozi la Merseyside kati ya miamba hao na Everton kusakatiwa Goodison Park.
Awali, Anderson alihofia uwezekano wa mashabiki kushindwa kujidhibiti na kukongamana nje ya uwanja wa Anfield, tukio ambalo lingezua rabsha, vurugu na makabiliano makali kati yao na maafisa wa usalama.
Hili ni jambo ambalo lingeenda kinyume na kanuni za afya zilizopo katika juhudi za kudhibiti maambukizi zaidi ya virusi vya homa kali ya corona.
Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) imeratibiwa kuanza upya mnamo Juni 17 bila mahudhurio ya mashabiki. Viwanja vitakapovyotumiwa na Liverpool kucheza dhidi ya Everton na mabingwa watetezi Manchester City bado havijathibitishwa.
“Tupo mahali pazuri na nafuu zaidi kuliko tulipokuwa wiki nne zilizopita. Dalili zote zinaashiria kwamba tunaelekea kufaulu kusadikisha mashabiki wetu kuhusu umuhimu wa kutokongamana nje ya uwanja wa Anfield wakati wa mechi dhidi ya Everton au Man-City,” akasema Anderson.
Hadi kipute cha EPL kiliposimamishwa kwa muda mnamo Machi 13, Liverpool walikuwa wakiselelea kileleni mwa jedwali kwa alama 82 huku pengo la pointi 25 likitamalaki kati yao na nambari mbili Man-City.
Mchuano wao wa kwanza kwa mujibu wa ratiba mpya ya EPL ni gozi dhidi ya Everton mnamo Juni 21. Ushindi kwa Liverpool katika pambano hilo utawahakikishia ufalme wa soka ya Uingereza kwa mara ya kwanza baada ya miaka 30.
Kati ya mechi ambazo zina historia ya kuwa kivutio kikubwa miongoni mwa mashabiki wa Liverpool ni gozi la Merseyside na kivumbi ambacho huwakutanisha na Man-City au Manchester United.
Maafisa wa usalama wanapendekeza haja ya kuandaliwa kwa michuano hiyo, ambayo kihistoria hushuhudia mahudhurio ya idadi kubwa ya mashabiki, katika viwanja mbadala visivyo vya nyumbani kwa kikosi chochote.
Aston Villa wataialika Sheffield United mnamo Juni 17 kabla ya Man-City kuvaana na Arsenal ugani Etihad siku hiyo hiyo. Mechi hizo mbili ni zile zilizokuwa zimesalia kwa vikosi hivyo kucheza ili kufikia idadi ya michuano 29 ambayo wapinzani wote wengine 16 walikuwa wamepiga hadi kipute hicho kilipositishwa kwa muda kutokana na janga la corona.
Mechi zote za raundi nzima ya 30 zimeratibiwa kusakatwa kati ya Ijumaa ya Juni 19 na Jumapili ya Juni 21. Jumla ya mechi 92 zimesalia kutandazwa katika EPL muhula huu.