Michezo

Mbappe, Sterling na Sancho waongoza kwa thamani ya wachezaji duniani

June 12th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

RAHEEM Sterling, Jadon Sancho, Trent Alexander-Arnold na Marcus Rashford ni miongoni mwa wachezaji watano wenye thamani ya juu zaidi kwa sasa katika soka ya bara Ulaya.

Orodha hiyo inaongozwa na nyota wa Paris Saint-Germain (PSG) na timu ya taifa ya Ufaransa, Kylian Mbappe, 21. Thamani ya Mbappe inakadiriwa sasa kufikia Sh32.3 bilioni.

Orodha hiyo iliyoandaliwa na shirika la CIES Football Observatory inalenga wanasoka wanaoshiriki Ligi Kuu tano za soka ya bara Ulaya, yaani Uingereza (EPL), Ujerumani (Bundesliga), Uhispania (La Liga), Ufaransa (Ligue 1) na Italia (Serie A).

Sogora matata wa Juventus na nahodha wa timu ya taifa ya Ureno, Cristiano Ronaldo, 35, ametupwa hadi nafasi ya 70 kwenye orodha hiyo.

Mnamo Februari 2020, CIES Football Observatory iliyo na makao makuu nchini Uswisi, ilisema kwamba Liverpool ndiyo klabu inayojivunia kikosi cha wachezaji wenye thamani kubwa zaidi duniani (Sh177 bilioni), mbele ya Manchester City (Sh173 bilioni) ambao wanashikilia nafasi ya pili.

Sterling, 25, ameingia katika orodha ya wanasoka wa haiba kubwa zaidi kambini na Man-City na timu ya taifa ya Uingereza tangu abanduke uwanjani Anfield alikokuwa akivalia jezi za Liverpool mnamo 2015.

Fowadi huyo anayemezewa mate na Real Madrid ya Uhispania anashikilia nafasi ya pili miongoni mwa wachezaji wenye thamani kubwa zaidi ulimwenguni (Sh24 bilioni) mbele ya Sancho (Sh22 bilioni). Huduma za Sancho ambaye kwa sasa ni kiungo wa Borussia Dortmund nchini Ujerumani, zinahemewa pakubwa na Manchester United.

Alexander-Arnold wa Liverpool, 21, anashikilia nafasi ya nne (Sh21 bilioni) mbele ya Rashford (Sh19 bilioni) ambaye amefungia Man-United jumla ya mabao 14 kutokana na mechi 22 za EPL msimu huu.

Miongoni mwa masuala yaliyozingatiwa na CIES katika kujumuisha orodha ya wanasoka wenye thamani kubwa zaidi duniani ni umri wao, matokeo yao katika ngazi za klabu na timu ya taifa na mfumo wa sasa wa usajili katika soko la uhamisho wa wachezaji.

WANASOKA 25 WA THAMANI KUBWA ZAIDI BARANI ULAYA

MCHEZAJI KLABU THAMANI

1 Kylian Mbappe PSG Sh32.3 bilioni

2 Raheem Sterling Man-City Sh24.2 bilioni

3 Jadon Sancho Dortmund Sh22.2 bilioni

4 Trent Alexander-Arnold Liverpool Sh21.2 bilioni

5 Marcus Rashford Man-United Sh19 bilioni

6 Mohamed Salah Liverpool Sh18 bilioni

7 Sadio Mane Liverpool Sh17.3 bilioni

8 Antoine Griezmann Barcelona Sh16.9 bilioni

9 Alphonso Davies Bayern Munich Sh16.6 bilioni

10 Harry Kane Tottenham Sh14.8 bilioni

11 Roberto Firmino Liverpool Sh14.8 bilioni

12 Bernardo Silva Man-City Sh14.2 bilioni

13 Gabriel Jesus Man-City Sh14.1 bilioni

14 Joao Felix Atletico Sh13.4 bilioni

15 Erling Haaland Dortmund Sh13.4 bilioni

16 Serge Gnabry Bayern Sh13.3 bilioni

17 Bruno Fernandes Man-United Sh13 bilioni

18 Matthijs de Ligt Juventus Sh13 bilioni

19 Mason Mount Chelsea Sh12.7 bilioni

20 Frenkie de Jong Barcelona Sh12.7 bilioni

21 Rodri Man-City Sh12.6 bilioni

22 Lionel Messi Barcelona Sh12.4 bilioni

23 Lautaro Martinez Inter Milan Sh12.3 bilioni

24 Virgil van Dijk Liverpool Sh12.3 bilioni

25 Saul Niguez Atletico Sh12.1 bilioni