SIHA NA LISHE: Vyakula muhimu kwa ubongo wa binadamu
Na MARGARET MAINA
UBONGO ndio unahakikisha viungo muhimu vya mwili vinafanya kazi ipasavyo.
Ubongo ni muhimu sana kwa afya ya mwanadamu na hivyo ni muhimu kuhakikisha kiungo hicho cha mwili kinapata virutubisho vifaavyo.
Ubongo huongoza kufanya kazi na kusonga kwa viungo vya mwili, mawazo, kumbukumbu za akilini na kuhakikisha viungo vya mwili vinafanya kazi ipasavyo kwa uwiano na ushirikiano unaostahili.
Samaki
Samaki huwa na virutubisho pamoja na mafuta ya Omega-3.
Asilimia kubwa ya ubongo wa binadamu ni mafuta.
Ubongo wa binadamu hutumia Omega-3 kutengeneza seli mpya. Mafuta hayo ni muhimu kwa kumwezesha mtu kujifunza kitu na kukumbuka.
Kahawa
Iwapo unakunywa kahawa asubuhi, utafurahia kusikia kuwa inafaa.
Viungo viwili vya kahawa – kafeini na chembechembe za molekuli zinazosaidia kuzuia mchanganyo wa kemikali zinazoweza kuharibu seli za mwili, kwa kitaalamu anti-oxidants – vinasaidia ubongo wako.
Pia kahawa inachangamsha na kuongeza viwango vya kemikali kwa jina serotonin inayomfanya mtu kujihisi akiwa na furaha.
Bizari manjano (Turmeric)
Kiungo cha curcumin kinachopatikana kwa bizari manjano kimethibitishwa kufaidi seli za ubongo, kupunguza msongo wa mawazo na kuboresha uwezo wa kukumbuka.
Brokoli
Brokoli au Broccoli ina viungo muhimu vinavyosaidia kuondoa sumu mwilini. Aidha, mboga hii imesheheni vitamini K ambayo utafiti umeonyesha huchangia kuboresha uwezo wa kukumbuka.
Chai ya kijani kibichi (Green Tea)
Viungo vya caffeine vya L-Theanine vinavyopatikana katika chai hii vinamsaidia mtu kujihisi akiwa mtulivu.
Chokoleti nyeusi
Chokoleti ina viungo vya flavonoids ambavyo ni muhimu kuboresha eneo la ubongo linalohusika na kukumbuka au kumbukumbu.
Pia ina viungo vya kafeini na vya kuzuia mchanganyo wa kemikali unaoweza kuziathiri seli, yaani anti-oxidants vinavyochangamsha ubongo.
Njugu
Njugu zimesheheni vitamini E na vitamini za kundi la B ambazo ni muhimu kwa kuboresha afya ya ubongo.
Vitamini E husadia ubongo wa mtu kuweza kuelewa lugha na mazungumzo pamoja na kumwezesha kuzungumza.
Machungwa
Machungwa yana vitamini C ambayo ni vitamini muhimu katika kuzuia kudumaa kwa ubongo na kukua kwa seli zake.
Machungwa yana kemikali ambayo husaidia kuimarisha ubongo wa mtu kukumbuka mambo upesi
Mayai
Mayai yana virutubisho muhimu vya ubongo ikiwemo vitamini B6 na B 12, folate na choline.
Mayai yana vitamini D ambayo ni muhimu kwa afya ya ubongo.