• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 5:36 PM
BURUDANI: Highland Academy Actors wana ari ya kutoa filamu kadhaa zenye mafunzo ya maadili mema

BURUDANI: Highland Academy Actors wana ari ya kutoa filamu kadhaa zenye mafunzo ya maadili mema

Na ABDULRAHMAN SHERIFF

MAKUNDI ya wasanii na hasa ya waigizaji yamekuwa yakianzishwa katika sehemu za kaunti ndogo za Kisauni, Nyali, Mvita, Changamwe, Old Town, Jomvu na Likoni kwa ajili ya kuinua vipaji vya waigizaji, wanenguaji na waimbaji.

Highland Academy Actors ni kimojawapo cha vikundi vilivyoanzishwa kwa ajili ya kuwafanya chipukizi wenye talanta ya uigizaji kuinua vipaji vyao kwa pamoja wakiwa na nia kubwa ya kutoa filamu ambazo wana imani kubwa zitaitikiwa na wapenda filamu.

Mwenyekiti wa kikundi hicho, Martha Wakoli anasema wamepania kuhakikisha wanatoa filamu kuhusu maisha wanayoishi masikini, mafunzo ya heshima kwa wazazi na watu wakubwa, malezi ya watoto mayatima, vichekesho na kusisitiza umuhimu wa elimu.

 

Mwenyekiti wa kikundi cha Highland Academy Actors Martha Wakoli. Picha/ Abdulrahman Sheriff

Mbali na hayo, kikundi hicho pia kina mipango ya baadhi yao kuwa wanenguaji, washairi na waimbaji.

“Tumeanzisha kikundi hichi kwa ajili ya kuwahusisha wavulana na wasichana wapate kujihusisha na usanii badala ya kukaa mitaani bila ya kuwa na ya kufanya,” akasema Martha.

Kinara huyo alisema wamekuwa tayari kutoa filamu inayojulikana kwa jina la ‘Rich family and poor family’ ambayo iko kwa Kiswahili japo jina la filamu yenyewe ni la lugha ya Kiingereza.

Martha aliishukuru shule ya St David’s High School na mwalimu mkuu Pascal Sultan kwa kuwaruhusu kufanyia mazoezi yao na pia kuwasaidia kwa njia nyingine ya ushauri wa jinsi ya kuendeleza kikundi chao.

Katibu wa kikundi hicho, Edith Irako anasema kuwa tayari wametayarisha filamu kadhaa ambazo kwa wakati huu wanasubiri kuzirekodi na kutayarisha sherehe ya kuzindua filamu yao ya kwanza.

Edith anasema kuwa wana wanachama 30 wenye umri kati ya miaka 11, Moses Daudi na mkubwa zaidi ni Dominic Omusula na Linus Supa wenye umri wa miaka 30 kila mmoja.

Katibu huyo alisema changamoto kubwa wanayokabili ni ukosefu wa udhamini na akatoa ombi kwa wahisani wajitokeze kuwasaidia ili vijana walioko kundini wapate kurekodi filamu zipatazo tano ambazo ziko tayari zinasubiri pesa za kurekodi.

“Kwa ajili ya kuwasaidia vijana wa sehemu tunayoishi ya Kaunti Ndogo ya Kisauni, tunawaomba wadhamini wakiwemo wafanya biashara na wanasiasa wa sehemu yetu na Mombasa na wahisani wajitokeze kutusaidia kukiimarisha kikundi chetu,” akasema Edith.

Jambo la busara zaidi ni kuwa kikundi hicho kina wasanii wa makabila mbalimbali na hii imetokana na uongozi kutaka kuwajumuisha wanachama wadumishe mapenzi kati yao na kueneza mapenzi hayo kwa familia zao na nyenginezo wanazoishi pamoja mitaani.

Wanachama wengine wa kundi hilo ni Brack Sidicy, Cynthia Achieng, Rose Vuguza, Saumu Muogobin, Issa Hamisi, Martin Pasaka, Said Mkamba, Fred Msembi, Roselyn Atieno, Elisha Yaah, Marita Wakoli, Linus Supa, Allan Mapigo, Ann Hussein na Penina Kisingo.

Wengine ni Mitchel Mumali, Dominic Omusula, Emmaculate Owino, Saumu Said, Purity Achieng, Cynthia Mmbone, Daisy Miroya, Edith Irako, Master Chiro, Pherus Khasandi, Moses Daudi na Zedi Mohamed.

Mkurugenzi wa kikundi cha Highland Academy Actors Daniel Odira. Picha/ Abdulrahman Sheriff

Mkurugenzi wa kikundi hicho, Daniel Odira ambaye pia ni msanii mwenye kipawa cha uchekeshaji alisema waliunda kikundi hicho Machi 2020 akiwa na Issa Hamisi, Cynthia Achieng, Edith Irako na Allan Mapigo.

“Tulianzisha kikundi hiki kwa madhumuni ya kuwafanya vijana wawe wenye kujihusisha na usanii sababu nilishuhudia sehemu hii kuwa na vipaji vya wasanii aina mbalimbali. Kwa wakati huu, tumeanza kwa kufanya filamu lakini karibu tutakuwa na kikundi cha wanenguaji,” akasema Odira.

You can share this post!

EPL: Ighalo asema wanajihisi wako tayari kikosini...

Wanasoka wa EPL sasa kuvalia jezi zenye maandishi...

adminleo