Michezo

SDT yahitaji majuma matatu kuamua hatima ya KPL

June 13th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

KLABU za Ligi Kuu ya Kenya (KPL) zitalazimika kusubiri zaidi hadi Juni 30, 2020 kujua iwapo kampeni za soka ya msimu huu zitarejelewa au la.

Hii ni baada ya Jopo la Mizozo ya Spoti (SDT) chini ya uenyekiti wa John Ohaga kusema kwamba linahitaji majuma matatu zaidi kufanya maamuzi muhimu kuhusu hatima ya KPL kutokana na mashtaka dhidi ya Shirikisho la Soka la Kenya (FKF).

Mbali na kuamua kesi inayohusu uhalali wa kuendelea kuwepo kwa maafisa wa FKF ofisini licha ya awamu yao ya uongozi kutamatika rasmi mnamo Februari 10, 2020, SDT pia inatazamiwa kuthamini uhalali wa hatua ya FKF kutamatisha ghafla kampeni za Ligi Kuu msimu huu bila kushauriana na kampuni ya KPL ambao ni waendeshaji wa kipute hicho.

Kesi kuhusiana na maamuzi hayo ya FKF iliwasilishwa na KPL kwa pamoja na kikosi cha Chemelil Sugar kilichoshushwa daraja na mabingwa wa 2006, SoNy Sugar. Nafasi za klabu hizo zilizoteremshwa zilitwaliwa na Nairobi City Stars na Bidco United waliopandishwa ngazi kutoka Ligi ya Kitaifa ya Supa (NSL).

Hata hivyo, SDT imeshikilia kwamba imedumisha kwa muda maamuzi ya FKF ya kutamatisha kampeni za KPL msimu huu kutokana na janga la corona na kutawaza Gor Mahia mabingwa wa msimu huu. Jina la Gor Mahia tayari limewasilishwa kwa Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) kuwa ndio watakaowakilisha Kenya kwenye kivumbi cha Klabu Bingwa Afrika (CAF Champions League) msimu ujao.

Katika malalamishi yao, KPL na Chemelil wanadai kwamba FKF haina mamlaka ya kufutilia mbali msimu wa Ligi Kuu wala kutawaza kikosi chochote mabingwa wa kipute hicho kwa kuwa awamu ya kuhudumu kwa Kamati Kuu Tendaji ya FKF na Rais wake Nick Mwendwa ilikamilika rasmi Februari 10.

KPL wanataka SDT ibatilishe maamuzi hayo ya FKF na kumshurutisha Mwendwa kuacha kuvuruga jitihada zao za kusimamia masuala yote ya uendeshaji wa Ligi Kuu ya Kenya.

KPL wanataka pia SDT itathmini uhalali wa mkataba wa 2015 uliotiwa saini na FKF na KPL na iwapo FKF ina mamlaka ya kutorefusha muda wa kuendesha kwao Ligi Kuu ya humu nchini baada ya Septemba 24, 2020.

Kwa upande wao, Chemelil wanadai kwamba hatua ya FKF kutawaza Gor Mahia mabingwa wa KPL mnamo Aprili 30, 2020 kumewaathiri pakubwa baada ya kuteremshwa ngazi hadi NSL.