• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 1:14 PM
Messi afunga Barcelona wakirejelea La Liga kwa kishindo

Messi afunga Barcelona wakirejelea La Liga kwa kishindo

Na CHRIS ADUNGO

BARCELONA walifunga bao katika sekunde ya 66 ya kurejelea kwao kampeni za Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) na kupata hamasa ya kuwapepeta Mallorca 4-0 mnamo Jumamosi usiku.

Kiungo mzawa wa Chile, Arturo Vidal aliwafungulia waajiri wake ukurasa wa mabao kabla ya fowadi wa zamani wa Middlesbrough, Martin Braithwaite kupachika wavuni goli lake la kwanza kambini mwa Barcelona.

Luis Suarez alitokea benchi katika mchuano uliokuwa wake wa kwanza tangu mwanzoni mwa Januari 2020 alipopata jeraha baya la goti. Beki Jordi Alba aliyafanya mambo kuwa 3-0 kunako dakika ya 79.

Nahodha Lionel Messi alifunga bao lake la 20 hadi kufikia sasa msimu huu katika dakika ya 90 na kuzamisha kabisa chombo cha Mallorca walioanza kipindi cha pili kwa matao ya juu.

Barcelona ambao ni mabingwa watetezi wa La Liga kwa sasa wanaselelea kileleni mwa jedwali kwa alama 61 huku pengo la pointi 11 likitamalaki kati yao na Sevilla wanaofunga orodha ya tatu-bora. Washindani wakuu wa Barcelona, Real Madrid, walikuwa jana wenyeji wa Eibar uwanjani Alfredo Di Stefano.

Likizo ya lazima iliyotokana na mlipuko wa corona, ilimpa Suarez, 33, fursa ya kupona baada ya straika huyo mzawa wa Uruguay kufanyiwa upasuaji kwenye goti lake la kulia mnamo Januari 2020.

Fowadi huyo wa zamani wa Liverpool alishirikiana vilivyo na Messi na akachangia bao la tatu kabla ya yeye mwenyewe kukosa nafasi kadhaa za wazi.

La Liga iliwapa Barcelona idhini ya kumsajili mchezaji wa ziada nje ya kipindi maalum cha uhamisho mnamo Februari 2020 baada ya mshambuliaji wao mzawa wa Ufaransa, Ousmane Dembele kupata jeraha baya ambalo lingemweka mkekani kwa kipindi kirefu. Ndipo miamba hao wa Uhispania wakamsajili Braithwaite kutoka Leganes.

Messi aliyachangia bao la Braithwaite, kwa sasa amechangia moja kwa moja mabao 15 kati ya 18 ambayo Barcelona wamepachika wavuni chini ya kocha mpya Quique Setien. Huu ni msimu wake wa 12 mfululizo kufungia Barcelona zaidi ya mabao 20 katika kipute cha La Liga.

You can share this post!

Mambo unayoweza kuachana nayo ili uwe mwenye furaha maishani

Corona yaingia Ikulu

adminleo