WAJIR: Kutoaminiana baina ya vikosi vya usalama na wakazi wa Khorof Harar kunahujumu usalama

Na FARHIYA HUSSEIN

SUALA la kutoaminiana baina ya vikosi vya usalama na wakazi wa Khorof Harar katika Kaunti ya Wajir limeonekana kama kizuizi kikuu katika kupambana na ukosefu wa usalama katika eneo hilo.

Wakazi hao wanalalamikia hofu ya kudhulumiwa kwa kushiriki habari na polisi.

Kijiji hicho kinachopatikana kilomita 20 mpakani mwa Kenya na Somalia kimefahamika sana kutokana na msururu wa mashambulio yanayotekelezwa na wapiganaji wa al-Shabaab.

Wakazi ambao wana wasiwasi wa kushambuliwa wakati wowote wanasema kwamba siku chache zilizopita, mfanyabiashara anayejulikana kama Gedi Abdi alichukuliwa na vikosi vya usalama katika eneo la Karsa.

Maafisa walimtuhumu mfanyabiashara wa eneo hilo kwa “kuwa na mkono katika shughuli za ugaidi.”

“Bw Abdi amekuwa akishirikiana na vitengo vya usalama. Pia wamekuwa wakiwazuilia wengine watano kwa siku tano sasa. Hatujui hata wanakozuiliwa,” alisema Ahmed Ismail, MCA wa eneo hilo.

Kulingana na mke wa mfanyabiashara huyo asiyejulikana aliko, Bi Maryan Bishar, idadi isiyojulikana ya watu ambao walikuwa na silaha na kudai kuwa ni kutoka kwa vikosi vya usalama walibisha mlango wa nyumba yake usiku mkuu.

“Walikuja hapa usiku mkuu na nilipofungua mlango walinielekezea bunduki na kuniamuru nitoke. Kisha wakaingia ndani ya nyumba wakitafuta vitu. Watoto wangu na majirani walibaki na mshangao nje. Sote tulishtuka na hakuna mtu aliyekuwa akituelezea nini kinaendelea,” akasema Bi Bishar.

Akaongeza: “Hata niliripoti suala hilo katika kituo cha polisi, hakuna kitu ambacho kimefuatiliwa.”

Wakazi hao wanasema wanaunga mkono juhudi za vikosi vya usalama kupambana na wapiganaji lakini wanapaswa kuepukana na kutumia nguvu nyingi hasa ikiwa mtu anashirikiana nao.

“Unapowafukuza wenyeji kwa nguvu au kuharibu mali zao, wanashtuka. Hii sio jinsi tunavyopaswa kushinda vita dhidi ya al-Shabaab,” alisema Musa Dimbil, mkazi mwingine.

Mzee wa kijiji katika eneo hilo Bw Ibrahim Kalmoy, anasema Bw Abdi alikuwa akishirikiana na vikosi vya usalama wakati wote alipokuwa akichunguzwa, lakini baadaye aliondolewa mashtaka yote baada ya kupatikana hana hatia.

“Yote ilianza na uvumi juu ya madai ya mfanyabiashara huyo alivyomiliki mali zake. Nilimchukua mwenyewe na kumpeleka kwa polisi wa kupambana na ugaidi mara mbili ambapo alichunguzwa na baadaye kuachiliwa. Pia wana rekodi zake katika ofisi zao,” akasema.

Wakazi sasa wanazihimiza vikosi vya usalama kuacha kutumia nguvu na badala yake wafanye uchunguzi wakidai kuwa maisha yao yako hatarini kutoka kwa polisi na wapiganaji wa al-Shabaab.