• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 3:23 PM
Msipuuze takwimu za mimba za wasichana – Serikali

Msipuuze takwimu za mimba za wasichana – Serikali

Na MWANDISHI WETU

SERIKALI Kuu imesema takwimu zilizoonyesha kuwa wasichana wadogo takriban 4,000 walitungwa mimba katika Kaunti ya Machakos tangu Januari hazifai kupuuzwa.

Kaimu Mkurugenzi wa Afya, Dkt Patrick Amoth jana alisema hayo alipotangaza serikali imeanzisha uchunguzi kuhusu ripoti iliyotolewa na Serikali ya Machakos kuhusu takwimu hizo.

“Utafiti kuhusu hali ya jamii nchini mwaka uliopita ulibainisha wasichana matineja takriban 400,000 hushika mimba kila mwaka kitaifa. Kwa hivyo inaweza kuaminika kama kaunti moja ina wasichana 4,000. Lakini tutachunguza takwimu hizo ndipo tufafanue zaidi kuzihusu,” akasema.

Takwimu hizo za wasichana 3,964 wenye umri wa kati ya miaka kumi hadi 19 waliopata uja uzito kuanzia Januari zilitangazwa na Afisa wa Watoto katika Kaunti ya Machakos, Bi Salome Muthama zikatiliwa mkazo na Gavana Alfred Mutua.

Zilishangaza wengi na kuibua mdahalo mkali, hasa ikizingatiwa jinsi wengine waliamini ni za kipindi cha Machi hadi Mei pekee wakati watoto wamekuwa nyumbani kwa sababu ya janga la corona.

Jana, Dkt Mutua alitoa wito kwa Rais Uhuru Kenyatta kuunda jopokazi maalumu kuchunguza na kutoa mapendekezo kuhusu jinsi ya kukabiliana na idadi kubwa ya wasichana wanaotungwa mimba nchini.

Vile vile, alitaka viongozi wa kidini watambue ukweli halisi uliopo katika jamii hasa kuhusu mienendo ya vijana, na waweke mikakati mipya kuwasaidia badala ya kutegemea maombi pekee.

“Wale waliopatikana ni walioshika mimba pekee. Tufikirie idadi yote ya watoto ambao wanatenda ngono bila kutumia kinga na hatari wanaojiwekea,” akasema.

Wakati huo huo, alitangaza kuunda jopokazi katika kaunti yake kuanzisha uchunguzi mara moja na kutoa mapendekezo ya kukabili suala hilo.

You can share this post!

Uhuru sasa aililia China ilegeze masharti ya madeni

Ruto ajinadi kwa miradi Uhuru akikwama Ikulu

adminleo