Habari MsetoSiasa

Bunge la Wajir laidhinisha mswada licha ya vurugu

June 19th, 2020 Kusoma ni dakika: 3

Na BRUHAN MAKONG

Bunge la Kaunti ya Wajir limeidhinisha mswada wa majina ya wanachama 11 walioteuliwa kuwakilisha Kamati ya Bajeti siku moja baada ya kizaazaa kushuhudiwa bungeni humo.

Baadhi ya wawakilishi wa wadi walizua vurugu siku ya Jumatano alasiri baada ya kutofautiana kuhusiana na uwakilishi wa kamati hiyo huku ndondi, makumbo na mateke yakishuhudiwa baina yao.

Hali hiyo iliwalazimu maafisa wa polisi kuingilia kati ili kusitisha mapigano hayo huku shughuli za bunge zikisitishwa hadi siku ya Alhamisi.

Wawakilishi hao walidai kuwa katiba ilikiukwa na baadhi ya wawakilishi wadi wakati wa kuwateua wanachama hao jambo ambalo liliwalazimu kupinga mswada huo.

Tukio hilo lililowaacha wakaazi wa kaunti hiyo vinywa wazi lilipelekea kujeruhiwa kwa watu wanne ikiwemo wawakilishi wadi.

Hata hivyo, mipango yao hayakufua dafu baada ya spika wa kaunti hiyo Ibrahim Yakub kuwafurusha kutoka majengo ya bunge kwa kukiuka sheria.

Inasemekana kuwa zaidi ya wawakilishi wadi saba walipewa adhabu ya kutoingia bungeni kwa siku ishirini na moja kutokana na tukio hilo.

Hapo jana, hali ilionekana tulivu huku askari wakipiga doria kwenye jengo hilo ili kuzuia kutokea kwa rabsha nyingine.

Hali tete pia ilishuhudiwa katika milango ya jengo la kaunti hilo baada ya wanahabari na wananchi kuzuiwa kuingia kwenye jengo hilo ili kushuhudia jinsi shughuli hiyo ilivyokuwa ikiendeshwa na bunge.

Hatua hiyo iliyopingwa vikali na baadhi ya wakaazi huku maswali mengi yakiibuka.

Baadhi ya wanahabari katika lango la bunge la kaunti ya Wajir walipozuiwa kufuatilia matukio ya bunge hilo siku ya Alhamisi. Picha/ Bruhan Makong

Bw Yakub alidai kuwa kuwepo kwa wanahabari kungepelekea vurugu zaidi baina ya wawakilishi wadi hao wakati wa shughuli hiyo.

Spika huyo aliongezea kuwa miongoni mwa sababu ya kuwakataza wanahabari fursa hiyo ilikuwa usalama wa wawakilishi wadi huku akiashiria kuwa kuwepo kwao pia kulikuwa tishio kwa usalama wa wakilishi wadi.

“Nilitoa agizo hilo kwasababu ya usalama wa wakilishi wadi,” alisema Bw Yakub. “Tunaipa kipaumbele usalama wa wakilishi wadi zaidi ya jambo jingine. Endapo itatokea kuwa sina uhakika na usalama wao basi ni jukumu langu na pia kwa manufaa yao na ya kaunti kuwazuia wanahabari kwenye jengo la kaunti,” aliongezea.

Hata hivyo baadhi ya wananchi waliyatilia shaka maelezo hayo huku wakijiuliza ni jambo lipi haswa liliendelea jengoni humo wakati wa shughuli hiyo wakidai kuwa hatua hiyo iliwekwa kwa minajili ya kuzuia uwazi na uwajibikaji.

Akizungumza na wanahabari Bw Yakub alisema kuwa tofuati na siku ya Jumatano ambapo vurugu ilishuhudiwa, wawakilishi wadi wote 30 waliokuwa bungeni siku ya Alhamisi waliunga mkono wanachama hao wapya.

“Kiwango chetu chenye tunahitaji kupitisha mswada wowote huwa 16 lakini siku ya leo wawakilishi wadi wote 30 waliokuwemo bungeni waliwaunga mkono wanachama wapya walioteuliwa,” alisema spika huyo.

Mwakilishi wadi wa Elben Mohamed Sheikh Ahmed alidai kuwa wale waliohusika na vurugu hapo awali hawakuwa na kura za kutosha lakini walisukumwa kuzuia shughuli hiyo na baadhi ya wanachama wa serikali ya kaunti hiyo ambao hawakufurahishwa na baadhi ya wanachama walioteuliwa.

“Baadhi ya majina yaliyoletwa bungeni yalionekana kama tishio na baadhi ya viongozi kwenye serikali ya kaunti. na wakati wowote endapo matarajio ya serikali ya kaunti na ya bunge yanaonekana kukinzana, sisi kama wawakilishi wadi ni wajibu wetu kuhakikisha kuwa tunaipa kipaumbele malengo yetu,” alisema.

Vuta ni kuvute kati ya bunge na serikali ya kaunti imekuwa ikishuhudiwa kwa muda sasa ikiwemo mwaka wa 2018 ambapo hali kama hii ilitokea baada ya wawakilishi wadi kutofautiana kuhusiana na uanachama wa bodi ya kuwaajiri wafanyikazi katika bunge hilo.

Polisi washika doria katika majengo ya kaunti ya Wajir siku ya Alhamisi. Picha/ Bruhan Makong.

Vita hivyo vya mara kwa mara vimeonekana kuwakera wakaazi ambao waliwanyoseha kidole cha lawama wawakilishi wadi hao kwa kushindwa kutekeleza maendeleo na kujali maslahi yao pekee huku wananchi wakiendelea kuhangaika.

Shukri Omar Abdi, mkaazi wa Wajir alisema kuwa wamechoshwa na jinsi wabunge hao wamekuwa wakiendesha shughuli za bunge hiyo huku akielezea kujuta kwao kwa kuwapigia kura viongozi hao.

Bw Abdi alitoa wito kwa mashirika ya kiserekali kuingilia kati na kupiga msasa mambo yanayofanyika jengoni humo yanayohusiana na wananchi.

“Wawakilishi wadi hawa wanapigania tu hali zao huku wakiwasahau wananchi. Akuna maendeleo yoyote tunayoyaona mashinani ilhali wananchi wanaendelea kuhangaika,” alisema Bw Shukri.

Mwakilishi wadi wa Tarbaj Issa Garore aliwapa changamoto serikali ya kaunti chini ya kamati ya fedha kuwakilisha hati muhimu yanayohusiana na shughuli za bunge la kaunti kwa wakati unaofaa kulingana na katiba ili kuzuia kuzuka kwa malumbano baina yao na wanachi