Mkutano wa Weta watibuliwa kwa vitoa machozi
BENSON AMADALA Na DERICK LUVEGA
POLISI Jumamosi walizima mkutano uliopangwa na kiongozi wa Ford Kenya Moses Wetang’ula nyumbani kwa mbunge wa Malava Malulu Injendi, kutoa mwelekeo wa kisiasa kwa jamii ya Waluhya kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022.
Polisi wa kukabiliana na fujo waliweka vizuizi katika barabara ya Kakamega-Malava, na kukatiza magari yaliyokuwa yakielekea nyumbani kwa mbunge huyo.
Wakati wa makabiliano hayo, polisi walilazimika kurusha vitoa machozi ili kutawanya umati nyumbani kwa mbunge huyo.
Baadaye, Bw Wetang’ula na kundi la wabunge walikutana katika Kakamega Sports Club kwa mashauriano.
Viongozi hao walikuwa awali wamehudhuria mazishi ya mama Sofia Monyo wa mbunge wa Luanda, Bw Christopher Omulele kabla ya kuelekea Kakamega.
Kamanda wa polisi eneo la Magharibi, Bi Peris Kimani alisema mkutano huo haungefanyika kwa sababu ulikiuka kanuni za kuzuia kusambaa wa virusi vya corona.
Akizungumza katika mazishi hayo, Bw Wetang’ula alisema kuwa yeye pamoja na kiongozi wa ANC, Musalia Mudavadi wanashinikiza ajenda ya eneo lenye umoja.
“Kuna watu ambao wanafikiria kuwa ukiwa hauko upande wao, uko upande ule wanaopinga,” alisema Bw Wetangula katika kile kilichoonekana kuwa jibu kwa kambi ya Bw Odinga ambayo imewahusisha na Naibu Rais William Ruto.
Aliendelea, “Tutakuunga vipi mkono wakati tuna mmoja wetu. Tunaeleza Waluhya wote kujua kuwa siasa ni za nyumbani.”
“Inapofikia kwa umoja wa jamii yetu, lazima kusiwe na mipaka kati ya jamii ndogo zetu 18 na vyama tunavyoshiriki,”aliongeza.
Naye Bw Injendi alisema hatua hiyo haitamtisha kamwe.
“Tumefanya uamuzi na tunajua kila uamuzi una athari zake. Hatutarudi nyuma katika azma ya kuunga mgombeaji urais tunayetaka,” alisema.
Awali katika mazishi hayo, Mbunge wa Alego Usonga, Samuel Atandi, alijipata matatani kwa kuwashutumu baadhi ya viongozi wa jamii ya Waluhya waliomlaumu kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga kwa kugawanya jamii hiyo.
Bw Atandi aliyemwakilisha Bw Odinga katika mazishi ya mama Sofia Monyo, alilazimika kukatiza hotuba yake huku vijana waliokuwa na hasira wakimzomea.
Mazishi hayo yalifanyika chini ya ulinzi mkali wa polisi waliokuwa na mbwa wa kunusa silaha.
Masaibu ya mbunge huyo yaliendelea huku vijana hao wakijaribu kumshambulia kwenye lango alipokuwa akiondoka.
Alilazimika kurudi katika uwanja ambao mazishi yalifanyika hadi polisi wakamuokoa.
Bw Omulele alifika katika lango kuwatuliza waombolezaji waliomvamia Bw Atandi wakimlaunu kwa kudharau viongozi wa jamii ya Waluhya.
Kwenye hotuba yake Bw Atandi alilaumu viongozi wa Waluhya kwa kujadili muungano wa jamii yao wakati nchi inapigana na janga la corona.
“Hali ya baadaye ya nchi hii haitegemei mnachofanya kama jamii,” alisema Bw Atandi aliyepuuza wito wa umoja wa Waluhya na kukasirisha waombolezaji.
Polisi walikuwa na wakati mgumu kuthibiti umati na wakawaruhusu kuhudhuria mazishi hayo lakini wakazuia wanahabari.