• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 8:50 AM
FUNGUKA: ‘Si uchawi, ni mapenzi’

FUNGUKA: ‘Si uchawi, ni mapenzi’

Na PAULINE ONGAJI

Siku kadhaa zilizopita nilikuwa nasikiza wimbo wa marehemu Remmy Ongala; Kipendacho Roho, kibao kilichonikumbusha maisha ya kaka mmoja kwa jina Resta niliyekutana naye miezi kadhaa iliyopita.

Kwanza kabisa hebu nikupe maelezo mafupi kumhusu. Resta ana miaka 35 na ni mfanyabiashara maarufu jijini Nairobi. Miaka mingi ambayo amedumu katika biashara imemzolea fedha na utajiri mkubwa.

Mbali na kufanikiwa kifedha, kimaumbile pia Mungu hakumnyima wema wake. Kamjalia utanashati unaojitokeza kupitia rangi yake ya chokoleti, umbo lake la miraba minne, na sura yake ya kupendeza.

Ni uzuri ambao bila shaka unaweza kumnasia binti yeyote amtakaye, lakini Resta ameamua kuingia katika uhusiano ambao kwa baadhi ya watu wanaomfahamu sio wa kawaida. Jicho la bwana huyu limenasa binti fulani kwa jina Cinta, afisa wa utawala ambapo wamekuwa wachumba kwa miaka sita sasa.

Miaka michache iliyopita Resta aligundua kuwa binti huyu alikuwa ni mke wa mtu na mama wa watoto watatu ambao alikuwa amewaficha eneo la mashambani.

“Niligundua kupitia simu niliyopokea kutoka kwa mwanamume aliyejitambulisha kama mumewe, akiniarifu kuwa Cinta alikuwa mkewe wa zaidi ya miaka sita na mama ya wanawe.

Jitihada zangu za kumuuliza kuhusu suala hili zimekuwa zikiambulia patupu, ambapo kila ninapojaribu kufanya hivyo, yeye hukasirika na kutishia kunitema.

Hata kuna wakati alinishambulia na kunijeruhi lakini sikumshtaki licha ya marafiki zangu kunirai kufanya hivyo.

Cha kushangaza ni kuwa muda unavyozidi kusonga ndivyo ninavyozidi kumpenda mwanamke huyu, kwani kichapo chake kimekuwa sumaku kwangu.

Isitoshe, kila ninapopata nafuu kutokana na majeraha ninayoyapata, mimi mwenyewe ndiye humtafuta.

Kuna wakati mmoja alinitishia kuniua na hata kuniitia majambazi nilipomuuliza kuhusu familia yake hiyo. Ni matukio yaliyowakasirisha jamaa zangu sana kiasi cha ndugu yangu kupiga ripoti polisi na kuhakikisha kwamba ametiwa nguvuni.

Wengi huniuliza kwa nini nimevumilia dhuluma hizi zote hasa ikizingatiwa kuwa ni mimi ninayeshughulikia mahitaji yake ya kifedha.

Kuna wale wanaosema kwamba binti huyu ametumia ushirikina kuninasa, lakini ukweli ni kwamba, ni mapenzi. Bibi huyu ananipa penzi bila kupima na yuko tayari kwenda hatua zozote zile kuniridhisha.

Kutokana na penzi hili, nimekubali kulishwa kwenye sinia moja na mumewe ambapo mimi humruhusu kwenda kwa mumewe kwa siku kadhaa kisha kurejea kwangu. Hata kuna wakati ambapo mumewe na wanawe huja kwangu kututembelea.

Jamaa na hata marafiki zangu wamefanya kila wawezalo kunitenganisha naye, lakini kwangu penzi hili linazidi kunoga kila kuchao”.

You can share this post!

Uhuru kuelekea Mlima Kenya kufufua umaarufu ulioyeyuka

Wanasiasa waanza harakati za kusaka mrithi wa Maraga

adminleo