Habari Mseto

Mjane ndani kwa kukata kuni

June 22nd, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na TITUS OMINDE

MAMA wa watoto 16 amehukumiwa kifungo cha miezi sita jela au kulipa faini ya Sh10,000 baada ya kupatikana na hatia ya kutema kuni katika msitu wa Turbo, Uasin Gishu kinyume cha sheria, mwishoni mwa juma.

Mjane huyo ni miongoni mwa watu watano kutoka vijiji vya Sango na Sipande katika kaunti-ndogo za Likuyani na Lugari ambao walihukumiwa jela mnamo Ijumaa baada ya kukiri hatia ya kupatikana na kuni kutoka kwa msitu huo.

Mahakama ya Eldoret iliambiwa kuwa mnamo Juni 15 katika kijiji cha Seregea na Sipande katika Kaunti ndogo ya Likuyani, Kaunti ya Kakamega, Eveline Nanjala alikamatwa akiwa na vipande vitano vya mti aina ya Pinus vyote vikiwa na thamani ya Sh16,000 bila idhini kutoka kwa Shirika la Huduma za Misitu nchini (KFS).

Nanjala, alikiri shtaka hilo mbele ya Hakimu Mwandamizi Mkuu wa Eldoret, Bw Richard Odenyo.

Akijitetea, aliambia mahakama kuwa yeye alikuwa mama mjane wa watoto 16, ambapo alikuwa amepokea mahindi kutoka kwa kiongozi wa eneo hilo kama chakula cha msaada kutokana na janga la virusi vya corona lakini hakuwa na kuni za kuwasha moto wa kuchemsha mahindi hayo ndiposa akaamua kwenda kusaka kuni msituni.

Baada ya kujitetea, mahakama ilimhukumu kifungo cha miezi sita au alipe faini ya Sh10,000.

Wengine waliokiri kosa sawa na hilo ni Paul Wafula ambaye alishtakiwa kwa kupatikana na magogo sita ya mti aina ya blue gum yenye thamani ya Sh30,000.

Wycliffe Lusweti kutoka kijiji cha Sipande alikiri kupatikana na vipande sita vya miti ya mbao yenye thamani ya Sh10,000.

Naye Ben Kulecho alikiri mashtaka ya kuwa na vipande vitatu vya miti vyenye thamani ya Sh15,000.

Vilevile, mshtakiwa mwingine Francis Shibaji pia alikiri kupatikana na vipande vinne vya mti aina ya blue gum ambavyo viliripotiwa kuwa vya thamani ya Sh12,000.

Washtakiwa hao pia walihukumiwa kifungo cha miezi sita jela au kulipa faini ya Sh10,000 kila mmoja.