• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 8:55 AM
Siku ya kivumbi Jubilee

Siku ya kivumbi Jubilee

Na CHARLES WASONGA

KIVUMBI kinatarajiwa Jumatatu katika mkutano wa wabunge wa chama cha Jubilee (PG) ambapo Rais Uhuru Kenyatta anatarajiwa kukamilisha mchakato wa ‘kusafisha’ chama kwa kuwatimua wandani wa naibu wake kutoka nyadhifa za uongozi bungeni.

Katika mkutano wa leo utakaofanyika katika jumba la KICC, Nairobi, Naibu Mwenyekiti wa Jubilee, Bw David Murathe ametaka wabunge wote wa Jubilee na vyama shirika wahudhurie mkutano huo akionya kuwa watakaosusia wataadhibiwa vikali.

“Yeyote asijaribu kukosa kuhudhuria mkutano wa kesho (leo) kwani atachukuliwa hatua ya kinidhamu kulingana na sheria ya chama cha Jubilee,” akasema katika taarifa fupi kwenye ukurasa wake wa Facebook.

Mkutano wa Juni 2, katika Ikulu ulihudhuriwa na wabunge 212 wa Jubilee, Kanu na vyama vingine vidogo vilivyounga Rais Kenyatta katika uchaguzi mkuu wa 2017.

Shoka linatarajiwa kumwangukia Kiongozi wa Wengi, Bw Aden Duale baada ya takriban wabunge 130 kutia saini hoja ya kutokuwa na imani naye.

Huenda nafasi yake ikapewa Mbunge wa Kipipiri, Bw Amos Kimunya, ambaye anapigiwa debe na mrengo wa wabunge waaminifu kwa Rais.

Kiranja wa Wengi, Bw Emmanuel Wangwe jana alisema hatima ya hoja hiyo iliyodhaminiwa na Mbunge wa Kieni, Bw Kanini Kega, itaamuliwa katika mkutano wa leo utakaoongozwa na Rais Kenyatta.

Katika mkutano wa kwanza uliofanyika katika Ikulu ya Nairobi mnmo Juni 2, 2020, Mbunge wa Mumias Mashariki, Bw Benjamin Washiali na Mbunge Maalum, Bi Cecily Mbarire walivuliwa nyadhifa za Kiranja na Naibu Kiranja wa Wengi, mtawalia.

Mbunge wa Kapseret, Bw Oscar Sudi alimsuta Bw Murathe kwa kuwazomea kama “watoto” kwa kuwashurutisha kuhudhuria mkutano wa PG.

“Sisi ni watu wazima na tulipokea mwaliko wa mkutano huo na bila shaka tutahudhuria kwa wingi tulivyofanya majuzi katika Ikulu ya Nairobi. Bw Murathe anafaa kutuheshimu,” akasema kupitia twitter.

Bw Wangwe alisema kuwa mkutano wa leo pia utatumiwa kuteua viongozi na wanachama wapya wa kamati zao bungeni zilizosalia wazi baada ya wabunge 16 kung’olewa katika nyadhifa walizoshikilia katika kamati hizo.

“Uongozi wa chama utajaza nafasi zilizobaki wazi kwenye kamati za bunge katika mkutano wa Jumatatu (leo) huku viongozi wapya wa kamati hiyo wakiteuliwa,” akasema.

“Hii ni kwa sababu sheria za bunge zinahitaji kuwa nafasi hizo zijazwe siku saba baada ya kusalia wazi,” akasema mbunge huyo wa Navakholo.

Bw Kega ni mmoja wa wale ambao wanakimezea mate kiti cha mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Bajeti kilichosalia wazi baada ya kubanduliwa kwa Mbunge wa Kikuyu, Bw Kimani Ichung’wa.

Naye Mbunge wa Moiben Silas Tiren anapigiwa upatu kupewa wadhifa wa mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Kilimo uliobaki wazi baada ya kutimuliwa kwa Mbunge wa Mandera Kusini, Bw Adan Haji.

Mkutano huu wa PG unajiri wakati ambapo ufa katika chama cha Jubilee umepanuka zaidi kufuatia hatua ya Dkt Ruto kuzindua kituo kipya cha Jubilee Asili, ambacho wabunge wandani wake wanasema ni mahala pao pa kukutana.

Wakiongozwa na Seneta wa Elgeyo Marakwet, Bw Kipchumba Murkomen, wabunge hao walidai kuwa waliamua kuzua wazo la kubuni kituo hicho baada ya kuzuiwa kufanya mikutano katika makao makuu ya Jubilee, eneo la Pangani, Nairobi.

“Tutakuwa tukijadili njia ya kutekeleza manifesto ya Jubilee na masuala mengi ya chama kutoka hapa. Sisi ndio tunaoshikilia sera na itikadi asilia ya Jubilee, chama ambacho tulijenga kwa bidii na moyo wa kujitolea,” akasema Bw Murkomen.

Alisema hayo baada ya Dkt Ruto kuongoza mkutano wa wabunge 16 waliofurushwa kutoka nafasi walizoshikilia katika kamati mbalimbali za bunge, akiwemo Bw Kimani ambaye alikuwa mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Fedha.

Lakini wandani wa Rais Kenyatta wakiongozwa na Bw Murathe wamefasiri hatua hiyo sawa na nia ya Naibu Rais kugura Jubilee na kubuni chama kipya cha kisiasa.

Viongozi kutokana eneo la Kaskazini Mashariki wakiongozwa na Seneta wa Garissa, Bw Yusuf Haji wamekuwa wakimhimiza Rais asimpokonye Duale wadhifa huo.

Lakini duru zimesema kuwa Rais Kenyatta tayari amekwisha kufanya uamuzi wa kumwondoa Mbunge huyo wa Garissa Mjini huku akipanga pia kutekeleza mabadiliko katika baraza la mawaziri na mashirika ya serikali.

You can share this post!

Mjane ndani kwa kukata kuni

Wakazi sasa wahofia mauaji ya kinyama ya watoto wa kike

adminleo