COVID-19 yazidi kuumiza wengi, utafiti waonyesha
Na BENSON MATHEKA
IDADI ya Wakenya wanaoshindwa kupata chakula kutokana na athari za janga la corona imeongezeka hadi asilimia 87, utafiti wa hivi punde wa kampuni ya infotrak unaonyesha.
Hali ni mbaya hivi kwamba Wakenya wanahisi kuwa wafungwa kufuatia marufuku na kanuni za kuzuia kusambaa kwa corona.
“Janga la corona limeathiri mapato ya watu. Tunaona wengi wakiendelea kuhangaika kuweka chakula mezani, kulipa bili za stima, maji na kwa jumla, mahangaiko yamezidi na sasa ni suala kuu,” alisema Bw Walter Nyabundi, Mkuu wa utafiti katika Infotrak alipotoa matokeo ya utafiti huo kupitia mtandao jana.
Kwa sababu ya kudidimia kwa mapato, asilimia ya watu wanaofanya kazi mijini hawatumi pesa kwa jamaa wanaowategemea maeneo ya mashambani jambo ambalo linaongeza wanaoteseka nchini.
Utafiti unaonyesha kwamba asilimia 67 ya Wakenya hawawezi kupata pesa za kununua dawa au kupata huduma za afya na asilimia 60 hawawezi kulipa kodi yote ya nyumba. Asilimia 63 walisema kwamba wanatatizika kulipa kodi kwa wakati.
“Kwa muda wa wiki chache zilizopita, mjadala kuhusu kodi ya nyumba umezidi, kwa upande mmoja, kuna wamiliki wa nyumba wanaozitegemea kwa riziki na upande mwingine kuna wapangaji wanaoshindwa kulipa kodi. Serikali nayo haina hakika kuhusu inayofaa kuunga katika suala hili,” alisema Bw Nyabundi.
Kulingana na utafiti huo ulioshirikisha watu 1200 kutoka kaunti 24, asilimia 75 ya Wakenya walisema kwamba hawawezi kulipa madeni yao kutokana na athari za janga la corona. Kufikia Jumamosi idadi ya watu waliothibitishwa kuwa na corona ilikuwa 4,478.
Watu 121 wameuawa na ugonjwa huo. Serikali inasema idadi ya maambukizi itazidi kuongezeka katika siku zijazo huku visa vikishuhudiwa maeneo tofauti ikiwemo Ikulu.
Watu wengi wamepoteza kazi baada ya sekta mbalimbali kuathiriwa na janga hilo. Utafiti wa infotrak unasema kwamba asilimia 68 ya Wakenya hawawezi kumudu bei ya makaa ya kupikia, mafuta taa na gesi na asilimia 54 ya watu wanaofanya kazi wanahangaika kwa kupunguziwa mishahara.
Ni asilimia 47 ya Wakenya waliosema kwamba wanategemea misaada ya chakula kutoka kwa wasamaria wema.
Kwa jumla, wanane katika kila Wakenya tisa wanafadhaishwa na janga la corona na nusu ya watu wanahisi presha ya hali ya sasa.
“Asilimia 36 ya Wakenya walisema kwamba wanatatizika kupata usingizi kutokana na janga hili,” utafiti unaeleza. Katika utafiti huo, Wakenya walisema kwamba wanamwamini zaidi waziri wa afya Mutahi Kagwe (asilimia 83 ) Rais Uhuru Kenyatta (asilimia 82 ) kwa habari kuhusu corona. Utafiti huo ulikuwa wa tatu kufanywa na kampuni hiyo kutathmini athari za corona