• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 6:55 AM
Hofu wakazi Mombasa wakipuuza sheria za kudhibiti corona

Hofu wakazi Mombasa wakipuuza sheria za kudhibiti corona

NA MISHI GONGO

MAAFISA wa afya katika kaunti ya Mombasa wameeleza hali ya wasiwasi kufuatia wakazi kuendelea kukiuka masharti yaliyowekwa na wizara ya afya licha ya idadi kubwa ya maambukizi ya ugonjwa wa COVID 19 katika eneo hilo.

Kulingana na mkuu wa afya ya umma, Bi Aisha Abubakar wakazi wamerudia maisha yao ya kawaida, wengi wakisusia kuvaa barakoa, kutokaribiana na kutumia viyeyuzi licha ya wizara ya afya kusisitiza sheria hizo.

Kulingana na takwimu kutoka kwa wizara ya afya eneo bunge la Mvita ndilo linaloongoza kwa idadi kubwa zaidi ya maambukizi.

Kufikia siku ya Jumamosi Mvita ilikuwa imeandikisha visa 453, Kisauni 189, Likoni 167, Nyali 147, Changamwe 134, na Jomvu ikirekodi visa 106.

Tangu kuzuka kwa ugonjwa wa COVID 19 nchini, Mombasa imeshikilia nambari ya pili katika kuwa na maambukizi mengi zaidi baada ya kaunti ya Nairobi.

Akizungumza katika mahojiano katika redio moja jijini humo mkuu huyo aliwaonya wakazi kuwa wasipozingatia maagizo basi virusi hivyo vitaendelea kuongezeka.

“Tunapaswa kufuata sheria zilizowekwa ili kujikinga sisi na familia zetu,” akasema.

Wakati huo huo, alisisitiza wanaojitenga majumbani mwao kuwa waangalifu na kuhakikisha kuwa hawaambukizi jamaa zao.

“Kuna baadhi ya watu ambao wameruhusiwa kujitenga majumbani mwao, hata hivyo kabla ya kuruhusu mtu kufanya hivyo lazima tuhakikishe kuwa anafuatilia maagizo ya wizara ya afya,” akasema.

Afisa huyo wa afya alitaja soko, vituo vya kuabiri magari na maskani kuwa miongoni mwa sehemu ambazo wakazi hawazingatii masharti yaliyowekwa ya kuvalia maski na kutokaribiana.

Aliongezea kuwa idadi kubwa ya watu bado wanadhania ugonjwa huo ni hadithi.

Mkuu huyo wa afya alisema tabia ya kutojali miongoni mwa wakazi ndio inayochangia katika kuongezeka kwa maambukizi.

Alitishia kuwa iwapo idadi ya maambukizi haitapungua basi serikali kuu inaweza kuweka sheria kali katika mji huo wa kitalii ili kudhibiti maambukizi.

Alisema asilimia 87 ya maambukizi katika mji huo ni ya waathiriwa ambao hawaonyeshi dalili ya kuwa na ugonjwa huo.

You can share this post!

COVID-19 yazidi kuumiza wengi, utafiti waonyesha

Sababu za kumng’oa Duale

adminleo