• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 10:55 AM
Sababu za kumng’oa Duale

Sababu za kumng’oa Duale

NA CHARLES WASONGA

CHAMA tawala cha Jubilee Jumatatu asubuhi kimemng’oa mbunge wa  Garissa Mjini Aden Duale kutoka wadhifa wa Kiongozi wa Wengi Bungeni katika mkutano wa wabunge wa chama hicho uliofanyika katika jengo la KICC, Nairobi.

Nasafi ya Bw Duale imechukuliwa na mbunge wa Kipipiri Bw Amos Kimunya huku wabunge 179 wakihudhuria mkutano huo.

Kinara wa chama hicho Rais Uhuru Kenyatta aliongoza mkutano huo huku naibu wake Dkt William Ruto pia akihudhuria baada ya onyo kali kutoka kwa naibu mwenyekiti wa chama hicho David Murathe dhidi ya kutohudhuria.

Kando na kuwa mwandani wa Naibu Rais William Rais shoka la Rais Uhuru Kenyatta lilimwangukia Aden Duale kutokana na tabia yake ya kuwashambulia hadharani mawaziri na maafisa wengine wakuu wa serikali.

Aidha, wabunge wanadai kuwa ilikuwa wazi kwamba Mbunge huyo wa Garissa Mjini alikuwa amepoteza imani ya wengi wao, haswa wale wanaunga mkono handisheki kati ya Rais na kiongozi wa ODM Raila Odinga.

Mbunge Mwakilishi wa Murang’a Sabina Chege Jumatatu alisema kuwa katika siku za hivi karibuni Bw Duale amekuwa akikiuka utaratibu uliopo kwa kushambulia bunge mawaziri bungeni kuhusiana na utendakazi wao.

“Kwa mfano, mwezi jana wakati wa mjadala kuhusu janga la Covid-19 bungeni Bw Duale aliongoza mashambulizi dhidi ya mawaziri George Magoha (Elimu), Fred Matiang’i (Usalama wa Ndani) na Inspekta Jenerali wa Polisi Hillary Mutyambai ilhali yeye ndiye anapaswa kutetea serikali,” akawaambia wanahabari katika jumba la KICC muda mfupi baada ya kutamatika kwa mkutano wa bunge wa Jubilee (PG).

Mbunge wa Kipipiri Amos Kimunya aliteuliwa kiongozi wa wengi huku Mbunge wa Eldas Aden Keynan akiteuliwa kuwa Katibu wa Kundi la Wabunge wa Muungano wa Jubilee, wadhifa ambao ulishikiliwa na Kimunya awali.

Kulingana na Bi Chege Bw Duale hakufaa kushambulia mawaziri hao moja kwa moja ndani ya bunge alipaswa kumfikia Rais Kenyatta kwa njia ya heshima na kumwarifu kuhusu utendakazi mbaya wa mawaziri wake.

“Katika hadhi yake kama kiongozi wa wengi ambaye ni macho na masikio ya Rais bungeni, Bw Duale hakupaswa kuonekana akiwashambulia mawaziri na maafisa wa serikali ambaye anapaswa kutetea,” akaeleza

Wakati wa mjadala huo kuhuusu Covid-19, Bw Duale alimkashifu vikali Bw Mutyambai kutokana na visa vya maafisa wa polisi kutumia nguvu kupita kiasi na kusababisha maafisa wakitekeleza sheria za kafyu.

“Bw Mutyambia hapaswi kuonekana kana kwamba anawajibu kwa Waziri Matiang’i ilhali anapaswa kuwajibikia Wakenya. Mauaji ya raia wakati wa kafyu inapasa kukoma. Ni aibu kwamba idadi ya watu waliouawa na polisi ni wakati huu ni ya juu kuliko wale walifariki kutokana na janga la Covid-19,” akasema Bw Duale.

Mbunge wa Tiaty William Kamket alidai wabunge walikosa imani na Bw Duale kutokana na tabia yake ya kuingilia na hata kuhujumu utendakazi wa kamati za bunge.

Huku akitoa mfano wa hatua ya Duale kuongoza kampeni ya kuongoza kampeni ya kutupiliwa mbali kwa ripoti ya Kamati ya Bunge kuhusu Elimu ambayo kuhusu uteuzi wa makamishna wapya wa Tume ya Huduma za Walimu (TSC).

“Kama kiongozi wa wengi hafai kuonekana kupinga ripoti za kamati za bunge kwa sababu yeye ni mmoja wa wale ambao hushiriki katika uteuzi wa uongozi wa kamati hizo. Hii ilimaanisha kuwa haheshimu kazi ambayo kamati za bunge zinafanya,” akasema na kuungwa mkono na Bi Chege.

Hata hivyo, wabunge tuliozungumza nao jana walisifu utendakazi wa Bw Duale kwa miaka saba ambayo amehudumu kama kiongozi wa wengi.

“Wakati wa hatamu yake, upande wa Serikali haijawahi kupoteza mswada au hata hoja yoyote. Isitoshe, Bw Duale amehakikisha watu wote walioteuliwa na Rais Kenyatta katika nyadhifa kuu serikali zimepita,” akasema Mbunge wa Lari Peter Mwathi.

Mkutano wa jana, sawa na ule wa Juni 2 katika Ikulu ya Nairobi, ulidumu kwa dakika 20 pekee. Baada ya Rais Kenyatta kuwasili ukumbini saa tatu na dakika 45 asubuhi shughuli zilianza ambapo ajenda ilikuwa ni moja pekee; uamuzi kuhusu hatima ya Bw Duale.

“Baada ya maombi, Katibu Mkuu Raphael Tuju alihutubu kwa dakika chache na akamwalika Rais. Na alianza kuwa kuuliza hivi: Mnataka Duale aendelee? Wabunge wengi wakajibu, ndio. Kisha akafichua kuwa amepokea hoja ya wabunge 126 wanaotaka Duale aondoke na Kimunya ashikilie,” akasema mbunge mmoja ambaye aliomba tulibane jina lake.

Mbunge huyo aliongeza kuwa Rais Kenyatta alitaja jina la Bw Kimunya kama chaguo la wengi na pendekezo hilo likaungwa mkono na mbunge wa kike kutoka Rift Valley.

“Na hapo mkutano ukaisha hivyo. Naibu Rais William Ruto ambaye pia alikuwepo hakupata nafasi ya kuhutubu,” akaongeza.

Licha ya wabunge wa mrengo wa tangatanga kutisha kuwa hawangehudhuria mkutano huo, wengi wao walikuwepo. Baadhi ya waliokuwepo ni Caleb Kositany (Soy), Moses Kuria (Gatundu Kusini), Esther Wahome (Kandara), miongoni mwa wengine.

Baada ya mkutano kumalizika, Bw Duale alidinda kuongea na wanahabari akisema; “Mtapata taarifa rasmi kutoka kwa viongozi wengine,”

Naye Bw Kositany akasema; “Leo hatuna stori. Mtapata stori kwa wale ambao wamepata viti.”

 

You can share this post!

Hofu wakazi Mombasa wakipuuza sheria za kudhibiti corona

Klopp na Ancelotti nguvu sawa

adminleo