Mutyambai kujibu maswali ya Wakenya kila Jumatatu kupitia Twitter
Na CHARLES WASONGA
INSPEKTA Jenerali wa Polisi Hillary Mutyambai ametangaza kuwa atakuwa akijibu maswali kutoka kwa umma mitandaoni kila Jumatatu kama sehemu ya juhudi za kushughulikia masuala yanayoibuliwa na umma kuhusu utendakazi wa maafisa wa polisi.
Bw Mutyambai alisema kumekuwa na shinikizo kutoka kwa umma za kutaka kubadilishana mawaidha na polisi na ndio maana ameamua kutenga saa moja kila Jumatatu kubadilishana mawazo na umma moja kwa moja kupitia Twitter.
“Huduma ya Kitaifa ya Polisi ina njia mbalimbali za kutangamana na umma. Vipindi kama hivi vitaimarisha ufanisi ya njia hizi. Kupitia vipindi kama hivi tutakuwa tukibadilishana mawazo kuhusu namna ya kuimarisha huduma zetu kwa umma,” akasema.
Bw Mutyambai alisema kupitia vipindi hivyo atakuwa akipokea mawaidha kutoka kwa umma kuhusu namna ya kuimarisha utendakazi wa maafisa wake.
“Vile vile, nitakuwa nikitambua suala ambayo yanapasa kushughulikiwa kwa dharura na afisi yake kulingana na matakwa ya umma,” akasema.
Kumekuwa na malalamishi kutoka kwa umma, tangu mlipuko wa Covid-19 utokee nchini, kuhusiana na mienendo ya maafisa wa polisi wanapohakikisha masharti ya kuzuia maambukizi ya virusi vya corona.
Visa vya maafisa wa polisi kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya wananchi vimekithiri katika sehemu mbalimbali nchini.
Zaidi ya watu 15 wameuawa na polisi wakihakikisha umma unatii sheria za kafyu na kanuni zingine za kuzuia maambukizi, kulingana na ripoti ya hivi majuzi iliyotolewa na Mamlaka Huru ya Kuchunguza Utendakazi wa Polisi (IPOA).
“Kando na watu 15 waliouawa wengine 31 wamejeruhiwa na maafisa wa polisi katika operesheni zao za kufanikisha utekelezaji wa sheria za kafyu,” ikasema ripoti hiyo iliyotiwa saini na Mwenyekiti wa IPOA Anne Makori.
Mamlaka hiyo pia imepokea ripoti 87 za malalamishi kutoka kwa umma kuhusiana na mienendo ya polisi tangu Machi mwaka huu.
Yassin Hussein Moyo, mvulana mwenye umri wa miaka 13 aliuawa na polisi katika veranda ya nyumba yao katika mtaa wa Huruma, Nairobi mnamo Aprili wakati wa utekelezaji wa sheria za kafyu.
Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Nordin Haji ameamuru kushtakiwa kwa afisa wa polisi aliyehusika na mauaji ya Yassin.