Habari

Kagwe asimulia jinsi anavyojizatiti Kenya ishinde janga la Covid-19

June 23rd, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na SAMMY WAWERU

NILIPOTEULIWA Waziri wa Afya sikutarajia ningekumbana na nyakati ngumu muda mfupi baadaye, hii ndiyo kauli ya Waziri wa Afya Mutahi Kagwe.

Bw Kagwe aliapishwa kuingia afisini Februari 28, 2020, ambapo alirithi mtangulizi wake Sicily Kariuki ambaye ni Waziri wa Maji.

Licha ya kuwa alifahamu masuala ya afya, Waziri Kagwe anasema hakuwa na ufahamu wowote kuhusu Covid-19.

“Sikujua kuhusu Covid-19 na ilibidi nianze kutafiti kuhusu ugonjwa huu ambao niliuskia Wuhan nchini China. Nilijua huenda ugonjwa huo ukaingia Kenya,” Kagwe alisema.

Akipigia upatu jitihada za wahudumu wa afya, Waziri hata hivyo alisema serikali haikuwa imepangia kuweka watu karantini ila ukiukaji wa mikakati na sheria zilizowekwa kudhibiti maambukizi uliilazimu kuizindua.

Huku maambukizi ya corona yakizidi kusajiliwa nchini, alisisitiza janga hili litadhibitiwa ikiwa wananchi watatii mikakati iliyowekwa na wizara ya afya.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Afya nchini, Dkt Patrick Amoth alikuwa ameonya kwamba kati ya mwezi Julai – Agosti, Kenya itashuhudia kiwango cha juu cha juu cha maambukizi ya Covid – 19.

Waziri Kagwe amesema ongezeko la idadi ya wagonjwa ni ishara kwamba kufikia mwishoni mwa mwezi huu wa Juni, huenda Kenya ikaandikisha zaidi ya visa 200 kila siku.

“Tulikuwa tumetabiri mwishoni mwa mwezi Julai, huenda sajili ikawa wagonjwa 200 kila siku. Sasa imeanza kuonekana takwimu zinazidi kuongezeka. Mwezi Julai kwa sababu watu huenda watasafiri sana, maambukizi yatakuwa juu,” akaonya.

Wakenya wakisubiri kuona iwapo Rais Uhuru Kenyatta atafunguashughuli pasina na zuio kamilifu na kulegeza masharti yaliyowekwa ifikapo Julai, Waziri Kagwe hata hivyo alisema hilo litategemea hali itakavyokuwa nchini na ulimwengu kwa jumla.

Pia, alisema grafu ya maambukizi na mienendo ya watu ndiyo itachochea Rais ama kufungua shughuli za uchumi kama kawaida au la.