Makala

SIKU YA WAJANE: Mjane aliye mhimili muhimu wa wajane na mayatima

June 23rd, 2020 Kusoma ni dakika: 3

Na SAMMY WAWERU

TABASAMU na ucheshi mara nyingi hufunika mengi mazito, machungu na magumu aliyopitia au hata anayopitia mtu maishani.

Rose Ndunge Mutiga ni mjane, mama wa watoto watatu. Mwanambee wake ana umri wa miaka 23, wa pili 22 na kifunga mimba akiwa na umri wa miaka 15.

Kifungua mimba na anayemfuata, wawili hao wako katika chuo kikuu.

Huku Kenya Jumanne, Juni 23, 2020, ikiungana na ulimwengu kuadhimisha Siku ya Wajane Duniani 2020, umbali aliofika Rose anasema ni kwa neema ya Mungu.

Rose anasema alifunga pingu za maisha 1996 kupitia harusi ya kanisa na mumewe alikuwa mhubiri.

Wawili hao walihakikisha watoto wao wanakua kwa msingi wa kufuata maadili bora.

Rose, 53, anasema ilikuwa ndoa ya aina yake katika jamii ila mwaka 2008 kifo kikampokonya mume.

“Mzee wangu aliugua kipindi kifupi akafariki. Hospitalini tuliambiwa aliugua homa ya matumbo, lakini baadaye ilibainika ni anemia,” anaeleza Rose.

Siku ya pili baada ya mume kuaga dunia, cheche za maneno yaliyozidisha majeraha moyoni mwake zilianza kurushwa.

“Mke wa ndugu ya mume tukiwa mochari alisema ‘mtu hawezi akafa hivyo kama kuku’, kwa hakika ni matamshi yaliyoumiza moyo,” anakumbuka.

Anasema matamshi hayo yalikuwa ishara ya mwanzo wa masaibu ya kuwa mjane.

Rose Ndunge Mutiga, licha ya kunyanyapaliwa akiwa mjane, ameibuka msaidizi mkuu wa wajane na mayatima. Picha/ Sammy Waweru

Kabla na wakati wa mazishi, dalili zilionyesha bayana kwa kina mume hakutakalika.

“Licha ya kuwa wazazi wa mume walikuwa wenye utu, nilichotaka ni amani. Baada ya kumzika mzee wangu, nilirejea jijini Nairobi tulikokuwa tukiishi,” anadokeza. Ikizingatiwa kwamba yeye ndiye alikuwa mama na baba wa wanawe, maisha yaligeuka kuwa shubiri.

Isitoshe, alikuwa amepoteza wazazi wake, lakini na aliamua kurejea alikozaliwa. Akidhania nyumbani, Kitui, ndiko amani ingepatikana, maji yalizidi unga.

Kilichoanza kama mzaha kudunishwa na mke wa kaka yake, hatimaye kilitunga usaha.

Rose anasimulia kwamba mvutano ulioibuka kati yao, uliishia kutatuliwa na wazee wa kijiji ambao walimuacha bila mbele wala nyuma.

“Uamuzi wa kikao hicho cha wazee ulichangia kufukuzwa nyumbani nilikozaliwa. Ghala la chakula – mazao na mavuno jasho langu – lilifungwa. Funguo za geti zikabadilishwa, nikawa nikirukia uani pamoja na wanangu. Kuingia jikoni na kuchota maji ya matangi ya maji vikawa marufuku. Nilipata msaada wa maji na chakula kupitia majirani,” mama huyo anaambia Taifa Leo.

“Nilikuwa nikisafiri masafa marefu kutafutia watoto angaa chakula, kupitia vibarua nilivyopokea Sh100 kwa siku,” anasema.

Ni unyanyapaa na masaibu aliyopitia kwa muda wa miaka miwili mfululizo, kabla kupata afueni.

Kupitia mama mmoja mwenye moyo wa kujali anayemiliki kituo cha watoto mayatima, 2010 Rose alirejea jijini Nairobi na wanawe kuanzisha upya maisha.

Rose Ndunge Mutiga (kulia), licha ya kunyanyapaliwa akiwa mjane, ameibuka msaidizi mkuu wa wajane na mayatima. Picha/ Sammy Waweru

Hata ingawa anauguza majeraha ya kumpoteza mume wake, changamoto chungu nzima zilizomkumba zilimnoa na kumpa taswira kamili ya pandashuka wanazopitia wajane.

Ni madhila yaliyomchochea mwaka 2015 aanzishe shirika lisilo la kiserikali, Bethel Widows & Orphans C.B.O, analosema limekuwa la manufaa tele kwa wajane na mayatima Nairobi.

“Shirika nililoanzisha linasaidia mayatima kupata wafadhili na hivyo kuwawezesha si tu kupata elimu, lakini pia kukidhi mahitaji ya kimsingi,” anafafanua.

Ni kupitia jitihada za shirika hilo, baadhi ya watoto mayatima eneobunge la Kasarani, Nairobi, hulipiwa karo kupitia hazina ya NG-CDF, chini ya afisi ya mbunge Mercy Gakuya.

Pia, Rose anasema wajane hupokea mikopo ya serikali kama vile Uwezo Fund, kupitia Bethel Widow and Orphan C.B.O, inayowawezesha kuanzisha biashara na pia kuiimarisha.

Dianah Kamande, mwasisi na mwanzilishi wa Come Together Widows and Orphans Organization – CTWOO, anasema ni muhimu wajane kujiunga na makundi au mashirika ya kijamii ili kupata mikopo ya serikali na pia ufadhili.

“Serikali haijui mtu binafsi. Serikali inajua makundi au mashirika, na hushirikiana na kufanya kazi na watu waliojipanga ili kuwainua kupitia mikopo na ufadhili. Mikopo itawawezesha kuanzisha biashara, kuiimarisha ili kujiendeleza kimaisha,” Dianah ambaye pia ni mjane anashauri.

Mbali na Uwezo Fund, wajane pia wanaweza kupokea mikopo kupitia Mpango wa Kuinua akina mama ndio Women Enterprise Fund for Women.

Unyanyapaa ni miongoni mwa changamoto wanazopitia wajane, jambo ambalo huchangia kunyang’anywa urithi wa mume.

Ni kiungo chocheo la maisha kuwa magumu, na Dianah anahimiza umuhimu wa kujiunga na makundi ya kijamii yanayoangazia wajane na mayatima.

Bethel Widow and Orphan C.B.O, shirika ambalo pia hutoa hamasisho kwa wajane kujiepusha kushiriki mienendo isiyofaa maishani, Rose anasema kwa sasa lina wajane 55 na takriban mayatima 200, wanaonufaika kulipitia.

Huku athari za janga la Covid – 19 zikiendelea kuhangaisha taifa, shirika hilo limejituma kutoa chakula cha msaada na mahitaji ya kimsingi kama vile barakoa, kupitia wafadhili wasamaria wema.

Rose, anahimiza wananchi kujitolea kusaidia wasiojiweza katika jamii, hasa nyakati hizi ngumu zinazosababishwa na virusi vya corona.

Anasema yeyote mwenye uwezo anaweza kuwasilisha msaada wake kwa shirika hilo kwa kuwasiliana na Rose Ndunge nambari ya simu: 0728498240