• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 11:13 AM
Klopp apinga pendekezo la gozi kati ya Manchester City na Liverpool kuchezewa kwingineko mbali na Etihad

Klopp apinga pendekezo la gozi kati ya Manchester City na Liverpool kuchezewa kwingineko mbali na Etihad

Na CHRIS ADUNGO

KOCHA Jurgen Klopp amepinga pendekezo la gozi la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kati yao na Manchester City kuchezewa katika uwanja tofauti usiokuwa Etihad ambao ni uga wa nyumbani wa wanasoka wa kocha Pep Guardiola.

Maamuzi kuhusu ama mechi hiyo itapigiwa uwanjani Etihad au kwingineko mnamo Julai 2, 2020, yatatolewa Alhamisi ya Juni 25 katika kikao kitakachoandaliwa na vinara wa soka ya EPL ugani Etihad.

Mechi kati ya Man-City na Liverpool ni miongoni mwa zile ambazo maafisa wa usalama jijini Manchester walikuwa wamependekeza zichezewe kwingineko kwa hofu kuepusha makabiliano makali kati ya polisi na mashabiki ambao watashawishika kukongamana nje ya uwanja.

“Ningependa mechi hiyo ichezewe Etihad. Vinginevyo, itakuwa vigumu sana kufanikisha maandalizi ya gozi lenyewe,” akatanguliza Klopp.

“Sijui jinsi itakavyokuwa, lakini nafahamu fika kwamba mchuano huo hautasakatiwa Anfield. Hivyo, itamaanisha kwamba Liverpool na Man-City watalazimika kusafiri kwingineko, jambo ambalo litahitaji kila kikosi kutafuta hoteli kwa gharama ambayo haikustahili kabisa,” akaongeza kocha huyo mzawa wa Ujerumani.

Liverpool wanaohitaji alama tano pekee kutokana na mechi nane zilizosalia katika EPL msimu huu ili kutwaa ufalme wa soka ya Uingereza kwa mara ya kwanza baada ya miaka 30, walipangiwa kuwa wageni wa Crystal Palace mnamo Juni 24, 2020.

Man-City ambao wanashikilia nafasi ya pili jedwalini kwa alama 20 nyuma ya Liverpool wameratibiwa kuwa wageni wa Chelsea uwanjani Stamford Bridge mnamo Juni 25, 2020.

Mojawapo ya michuano mingine iliyokuwa imepangiwa kuchezewa mbali kabisa na uwanja wa Goodison Park, ni gozi la Merseyside lililowakutanisha Liverpool na Everton mnamo Juni 21.

Hata hivyo, mechi hiyo ilipigiwa baadaye katika uga wa nyumbani wa Everton baada ya kuandaliwa kwa kikao kilichoshuhudia maafikiano kati ya serikali ya Uingereza, polisi na maafisa wa kipute cha EPL.

“Sioni haja ya kulazimisha vikosi kusafiri kwingineko kwa gharama za ziada. Hadi kufikia sasa, tangu mechi za EPL zirejelewe mnamo Juni 17, imebainika kwamba mashabiki wa EPL wanaelewa hali ilivyo na mabadiliko ambayo yameletwa na janga la corona kiasi kwamba wanafahamu wajibu wao katika juhudi za kukabiliana na maambukizi ya ugonjwa huu wa Covid-19,” akasema Klopp.

You can share this post!

Raila hajaenda ng’ambo kwa matibabu – ODM

Serikali yalenga kuhakikisha vijana wengi Kigumo wanapata...

adminleo