• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 12:45 AM
MARTHA ATIENO: Wasanii chipukizi wanaosaka ajira ni wengi

MARTHA ATIENO: Wasanii chipukizi wanaosaka ajira ni wengi

Na JOHN KIMWERE

AMEORODHESHWA kati ya waigizaji wa kike wanaokuja hapa nchini wakilenga kutinga hadhi ya kimataifa miaka ijayo. Ingawa hajapata umaarufu katika sekta ya uigizaji anasema analenga kukaza buti kuhakikisha anashiriki filamu zitakaofaulu kuonyeshwa kwenye runinga.

Martha Hellen Atieno ambaye kwa jina la msimbo anafahamika kama Andau anaamini anatosha mboga katika masuala ya maigizo.

Dada huyu aliyedhamiria kuhitimu kuwa mwalimu anasema alianza kushiriki maigizo kanisani alipoigiza mchezo kuhusu kuzaliwa kwa Yesu Kristo.

”Pia nikiwa Shule ya Upili nilikuwa nikishiriki michezo ya kuigiza ambapo wakati mmoja niliibuka mwana maigizo bora hali iliyonitia motisha zaidi katika sekta ya uigizaji,” anasema na kuongeza katika maisha yake uigizaji ndio tegemeo lake.

Kadhalika anasema licha ya kwamba hajapiga hatua kubwa katika uigizaji amepania kujituma mithili ya mchwa kuhakikisha anatinga kiwango cha waigizaji wa filamu za Kinigeria (Nollywood). Anatamani kufikia upeo wake msanii, Patience Ozokwor anayejivunia kushiriki filamu kama:’Blood Sister,’ ‘Mothers in Law,’ ‘Chied Daddy,’ ‘Alice my first Lady,’ na ‘Marcus D Millionaire’ kati ya zingine. ”Kadhalika natamani sana kuanzisha brandi yangu ya kuzalisha filamu ili nikuze wasanii chipukizi,” akasema. 

Kwa waigizaji wa anatamani sana kufanya kazi na waigizaji kama Grace Muna (Venesa) ‘Aunty boss,’ na Celestine Gachuhi ‘Selina,’ kati ya wengine.

Kisura huyu amekuwa katika tasnia ya uigizaji kwa miaka 12 anakojivunia kushiriki zaidi ya filamu kumi wala hana ajira nyingine.

Baadhi ya filamu ambazo ameshiriki ni kama: ‘Jaboya,’ ‘The Gods of the Rain,’ ‘Stubborn daugther,’ ‘Full stop,’ ‘Amina,’ Kavunja,’ na ‘Something to loose,” kati ya zingine.

Katika mpango mzima anajivunia kushiriki filamu kadhaa mwaka uliyopita zilizotenezwa chini ya ushirikiano wa kundi la GPAY Afrika na Cinemadamare Film Festival kutoka Italia. Ni zoezi lililowakutanisha wasanii wengi tu wa humu nchini na wenzao kutoka Italia. Kipindi hicho walitembelea Kaunti kadhaa ikiwamo Nairobi, Kisumu, Nyandarua, Makueni na Mombasa walikotegeneza filamu tofauti.

Msichana huyu anajivunia kufanya kazi na makundi kadhaa hapa nchini ikiwamo Ana kwa ana, Zuia Theatres Production, Tamasha Arts Production, Goodspell Theatres na GPAY Africa.

Kisura huyu anatoa mwito kwa waigizaji waliotangulia kuwashika mkono wenzao wanaoibukia maana wamefurika kote nchini wala hawajapata mwelekeo.

”Kusema kweli wasanii chipukizi ni wengi wanaosaka ajira,” alisema. Pia amesema serikali inastahili kuwa mstari wa kwanza kukuza waigizaji hasa kutoa sapoti kwa wasanii wanaokuja pia kuanzisha mikakati ya kuuza filamu za Kenya katika mataifa ya kigeni.

Mwigizaji huyu anashukuru viongozi wa GPAY Afrika, Samuel Oluoko na Amyn Khan kwa kuandaa zoezi hilo lililotoa nafasi kwa wasanii wa Kenya kushiriki filamu hizo. Aidha anashukuru mamake mzazi, Rebecca Achieng kwa kumshika mkono kwenye juhudi za kukuza talanta yake katika tasnia ya maigizo bila kusahau production zote zilizowahi kumpa nafasi ya kushiriki filamu mbali mbali.

You can share this post!

MARY MUSYOKA: Lupita Ny’ong’o hunitia moyo

LOSFOU: Nalenga kumfikia Diamond Platnumz

adminleo